Radio Fortune Africa -Na Cantona Joseph
https://liveonlineradio.net/radio-fortune-africa
Iran imetekeleza mashambulizi makubwa dhidi ya Israel kwa kutumia makombora ya balistiki. Makombora mengi yamenaswa, haswa katika anga ya Jerusalem na Tel Aviv. Lakini majeraha madogo mawili yaliripotiwa. Jeshi la Israeli limezungumzia juu ya kuongezeka kwa uhasama “mbaya na hatari”, hali ambayo itakuwa na athari kubwa. Tehran inasema iko tayari kupiga “miundombinu yote ya Israeli” ikiwa serikali ya Kiyahudi italipiza kisasi.

Iran inasema shambulio hilo la makombora ni la kulipiza kisasi mauaji ya mwezi Julai ya kiongozi wa Hamas, Ismail Haniyeh, pamoja na kiongozi wa Hezbollah, Hassan Nasrallah, siku ya Ijumaa – na kwa mauaji ya watu wa Lebanon na Wapalestina.
Televisheni ya taifa ya Iran imeangazia taarifa kutoka kwa IRGC (lslamic Revolution Guard Corps) ikithibitisha kuwa “makumi” ya makombora yamerushwa kuelekea Israel, na kutishia shambulio jingine iwapo Israel itajibu.
Wizara ya mambo ya nje ya Iran imelitaka baraza la usalama la Umoja wa Mataifa lichukue hatua za maana kuepusha vitisho dhidi ya amani na usalama wa Mashariki ya Kati.
Msemaji wa jeshi la Israel Daniel Hagari amesema shambulizi la makombora kiasi 180 lililofanywa na Iran jana Jumanne lilinuia kuwaua maalfu ya raia wa Israel na halikuwa la kawaida na wala halikutarajiwa. Jeshi la Israel pia limelilaani shambulizi hilo likiliita kuwa ongezeko baya na la hatari la machafuko. Hagari amesema Iran na washirika wake wanataka kuingamiza Israel na kutakuwa na matokeo na hatua za kujibu shambulizi hilo.
Rais wa Marekani Joe Biden amesema Marekani inaiunga mkono kikamilifu Israel kufutia shambulizi hilo la makombora ya masafa marefu, akilieleza kuwa limeshindwa na lisilo na tija yoyote. Akizungumza na waandishi habari katika ikulu yake mjini Washington, Biden amesema kuna mazungumzo yanayoendelea kuhusu jinsi Israel itakavyojibu shambulizi la Iran na kwamba athari kwa serikali ya mjini Tehran zitaonekana. Biden amesema atazungumza na waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu.
Nayo inasema sera ya Marekani kuelekea Mashariki ya Kati imeshindwa kabisa. Msemaji wa wizara ya mambo ya nje wa Urusi Maria Zakharova amesema katika taarifa yake aliyoiandika kwenye mtandao wa Telegram kwamba utawala wa rais Biden umefeli Mashariki ya Kati na kinachoendelea ni tamthilia ya umwagaji damu inayoendelea kushika kasi. Ameongeza kusema kauli zisizoeleweka za ikulu ya Marekani zinaonyesha Marekani iko katika hali ya kutokuwa na msaada kabisa katika kuitafutia ufumbuzi migogoro.
Radio Fortune Africa -Na Cantona Joseph
Discover more from cantonadigital
Subscribe to get the latest posts sent to your email.