Israel na Hezbollah zapambana katika mapigano ya ardhini ndani ya Lebanon
Radio Fortune Africa -Na Cantona Joseph
https://liveonlineradio.net/radio-fortune-africa
Baada ya kuripoti makabiliano ya moja kwa moja ndani ya Lebanon, Israel yathibitisha kifo cha mwanajeshi wake.
Muhtasari
- Israel yathibitisha kifo cha mwanajeshi wake wa kwanza tangu uvamizi wa Lebanon
- Abiria 100 hawajulikani walipo kufuatia ajali ya boti Nigeria
- Hezbollah yatangaza kukabiliana upya na wanajeshi wa Israel
- Israel yampiga marufuku katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini humo
- Iran: Khamenei azisuta nchi za magharibi baada ya kuishambulia Israel
- Jeshi la Sudan laapa kuendelea kupigana licha ya juhudi za amani
- Roketi takriban 100 zimerushwa kaskazini mwa Israel leo asubuhi
- Israel yatuma wanajeshi zaidi katika operesheni ya ardhini ya Lebanon
- Sean ‘Diddy’ Combs akabiliwa na madai mapya zaidi ya 100 ya unyanyasaji
- Mvutano unazidi kuongezeka Mashariki ya Kati huku mashambulizi yakiendelea
- Bei ya mafuta yapanda baada ya shambulizi la Iran
- Iran yanasema inaweza kuishambulia “miundombinu yote ya Israeli” ikiwa Israeli italipiza kisasi
- Tazama: Video inayoonyesha mashambulizi ya makombora ya Iran nchini Israel
- Marekani yasema iliisaidia Israel kuyadungua makombora ya Iran
- Netanyahu asema Iran italipia mashambulizi ya makombora, huku Israel ikianzisha mashambulizi mapya Beirut
Hezbollah yadai kuisababishia hasara jeshi la Israel
Kundi la Hezbollah linadai kuwa wapiganaji wake wamekabiliana na wanajeshi wa Israel ambao walikuwa wakijaribu kuzunguka kijiji cha Yaroun, kusini mwa Lebanon.
Hezbollah inasema wapiganaji wake “waliwashambulia” wanajeshi wa Israel kwa kilipuzi na kusababisha “maafa”.
Haya ni makabiliano ya pili wa moja kwa moja ambayo Hezbollah imedai kufanya.
Hapo awali, kundi hilo lilisema kuwa lilipambana na jeshi la Israel wakati “lilipovamia” mji wa Maroun al-Ras nchini Lebanon – ambao uko umbali wa kilomita 5 kaskazini mashariki mwa Yaroun.
Shambulio hili na mengine hayajathibitishwa na jeshi la Israel.
Lakini pande zote mbili sasa zimeripoti kupambana ”karibu” hii leo.
Netanyahu afanya mazungumzo na wakuu wa usalama
Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu amefanya mashauriano na wakuu wa usalama leo mchana mjini Tel Aviv.
Katika picha hapa chini, anaweza kuonekana ameketi mkabala na Waziri wa Ulinzi Yoav Gallant miongoni mwa wengine.
Netanyahu hapo awali aliapa kuijibu hatua Iran, akielezea shambulio hilo kubwa la jana usiku kama “kosa kubwa” ambalo Tehran “itajutia”.
Urusi yadai kuuteka mji wa Vuhledar mashariki mwa Ukraine

Wanajeshi wa Urusi wameudhibiti kikamilifu mji wa mashariki wa Vuhledar, ambao wanajeshi wa Ukraine wamekuwa wakiulinda tangu kuanza kwa uvamizi wa Moscow miaka miwili na nusu iliyopita.
Kamandi ya kijeshi ya mashariki mwa Ukraine ilithibitisha Jumatano kwamba iliwaambia wanajeshi ambao bado wanapigana katika sehemu za Vuhledar warudi nyuma ili wasije wakazingirwa.
Kwa zaidi ya miaka miwili Urusi imekuwa ikijaribu kuuteka mji huu ili kusonga mbele upande wa kaskazini na kufikia vituo vya usafirishaji vya kikanda kama Kurakhove na Pokrovsk.
Wanablogu wa kijeshi wanaoiunga mkono Kremlin walikuwa wamechapisha video kadhaa siku moja kabla ya kuwaonyesha wanajeshi wa Urusi wakiwa na bendera kwenye paa za majengo tofauti ya mji wa Vuhledar.
Israel yathibitisha kifo cha mwanajeshi wake wa kwanza tangu uvamizi wa Lebanon

Mwanajeshi wa kwanza wa Israel amethibitishwa kuuawa ndani ya Lebanon tangu uvamizi wa ardhini kuanza.
Jeshi la Ulinzi la Israel (IDF) lilitangaza katika taarifa kwamba Kapteni Eitan Yitzhak Oster, 22, aliuawa ndani ya Lebanon siku ya Jumatano.
Kijana huyo mwenye umri wa miaka 22 alikuwa katika kitengo cha Egoz, cha makomando maalumu wa vita vya ardhini, IDF inasema.
Awali IDF iliripoti kuwa “inapigana maeneo kadhaa” kusini mwa Lebanon.
“Jeshi la Wanahewa la Israeli, waliwatimua magaidi na kuharibu miundombinu ya kigaidi kwa mabomu yaliyoongozwa kwa usahihi na ushirikiano ya karibu.”
Taarifa hiyo inaongeza “zaidi ya miundombinu 150 ya ugaidi” imeharibiwa na katika mashambulizi ya hivi majuzi.
Abiria 100 hawajulikani walipo kufuatia ajali ya boti Nigeria
Mamlaka katika jimbo la Niger ya Kati nchini Nigeria wamesema takriban abiria 100 hawajulikani walipo baada ya ajali ya boti iliyotokea jana usiku kwenye mto Niger.
Boti hiyo ilikuwa safarini kutoka Mundi ikiwa na zaidi ya abiria 300, wengi wao wakiwa wanawake na watoto.
Ripoti za vyombo vya habari nchini humo zinasema takriban miili 60 ilipatikana baada ya ajali hiyo.
Abiria wengi walisemekana kuhudhuria tamasha la Waislamu, sherehe za Maulid huko Gbajibo.
Mkuu wa Shirika la Usimamizi wa Dharura wa Jimbo la Niger Abdullahi Baba Arah alisema katika taarifa kwamba mamlaka hiyo imeanza kufuatilia shughuli za utafutaji na uokoaji kwa kutumia watu wa kujitolea na wazamiaji wa ndani.
Bw. Baba Arah alisema kuwa mwitikio wa haraka kutoka kwa wafanyakazi wa kujitolea wa jamii umewezesha zaidi ya watu 150 kuokolewa kufikia sasa.
Alieleza kuwa shughuli ya uokoaji bado inaendelea ili kupata manusura zaidi.
Chanzo cha ajali hiyo hakijajulikana. Hata hivyo matukio ya kupinduka kwa boti katika Mto Niger ni ya kawaida hasa msimu wa mvua ambao hufanya kiwango cha maji mtoni kupanda.
Hezbollah yasema mapigano ya leo ni ‘awamu ya kwanza’ ya vita
Msemaji wa Hezbollah anasema mapambano yao ya leo dhidi ya Jeshi la Ulinzi la Israel kusini mwa Lebanon ni sehemu ya “duru ya kwanza ya vita”.
“Vikosi vyetu na wapiganaji wamejiandaa kikamilifu kukabiliana na adui,” Mohammad Afif wa Hezbollah aliwaambia waandishi wa habari, kama alivyonukuliwa na mashirik aya habari ya Reuters na NBC.
Afif anaongeza kuwa kundi hilo la wanamgambo lina silaha za kutosha kwa makabiliano na IDF.
Hezbollah na IDF wote wanaripoti mapigano ya ardhini ndani ya Lebanon siku ya Jumatano.
Hezbollah imetangaza hatuao hiyo baada ya wanajeshi wa Israel “kuvamia” mji wa Maroun al-Ras nchini Lebanon.
Mji huo uko karibu kilomita mbili kutoka mpaka wa Israeli-Lebanon.
Kwa mujibu wa Hezbollah, wanajeshi wa Israel waliingia kutoka upande wa mashariki, na mapigano yanaendelea, ilisema saa moja iliyopita.
Haya ni makabiliano ya pili ya moja kwa moja na wanajeshi wa Israel ambayo Hezbollah imedai leo.
Hapo awali, kundi hilo lilisema limefanikiwa kuzima uvamizi wa Israel nchini Lebanon.
Israel yampiga marufuku katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini humo

Waziri wa mambo ya nje wa Israel anasema Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres ”Hana ruhusa” kuingia Israel na amepigwa marufuku nchini humo.
Israel Katz anasema uamuzi wake unafuatia hatua ya Guterres “kutolaani” shambulio la kombora la Iran dhidi ya Israel siku ya Jumanne.
Anamshutumu mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa kwa kuwa “mpinzani wa Israel” na kutoa “msaada kwa magaidi, wabakaji na wauaji.Guterres atakumbukwa kama doa katika historia ya Umoja wa Mataifa kwa vizazi vijavyo.”
Jana, mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa alilaani “kuongezeka kwa mzozo wa Mashariki ya Kati” na kutoa wito wa kusitishwa kwa mapigano.
Iran: Khamenei azisuta nchi za magharibi baada ya kuishambulia Israel

Kiongozi mkuu wa Iran, Ayatollah Ali Khamenei, leo amekutana na kundi la wataalamu mjini Tehran.
Aliilaumu “Marekani na baadhi ya nchi za Ulaya” ambazo “zinadai kuleta amani na utulivu Mashariki ya Kati,” kwa kuchochea mvutano wa kikanda na vita katika eneo hilo.
Alisema lazima “watokomee” kutoka eneo hilo ili nchi za Mashariki ya Kati ziweze kuishi kwa amani.
Alisema kuwa “anaomboleza” kifo cha Kiongozi wa Hezbollah Hassan Nasrallah, lakini hakuahirisha mkutano wake na wataalamukwa sababu maombolezo ya Iran ni nguvu ya “kuhuisha na kuendesha”.
Agizo la kurusha makombora huko Israel siku ya Jumanne lilitolewa na kiongozi mkuu wa nchi hiyo – ambaye bado yuko katika eneo salama, afisa mkuu wa Iran aliliambia shirika la habari la Reuters.
Jeshi la Sudan laapa kuendelea kupigana licha ya juhudi za amani

Jenerali wa ngazi ya juu wa Sudan amesema jeshi litaendelea na mashambulizi yake licha ya juhudi za kimataifa za kukomesha mapigano katika vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyodumu kwa miezi 17.
“Mazungumzo ya amani yanaweza kuendelea, lakini jeshi halitasitisha shughuli zake kwa sababu ya hilo,” Msaidizi wa Kamanda Mkuu Luteni Jenerali Ibrahim Gabir aliiambia BBC.
Alikuwa akizungumza siku chache tu baada ya jeshi kuanzisha operesheni ya kuchukuwa udhibiti wa mji mkuu, Khartoum, kutoka kwa waasi wa RSF.
Pande hizo mbili zimekuwa zikipigana tangu Aprili mwaka jana, baada ya viongozi wao kufautiana kuhusu mustakabali wa nchi.
Mzozo huo umesababisha janga la kibinadamu huku zaidi ya nusu ya nchi ikikabiliwa na njaa na mamilioni ya watu kulazimika kuyahama makazi yao.
Roketi takriban 100 zarushwa kaskazini mwa Israel leo asubuhi

Ving’ora vya tahadhari kuhusu mashambulizi ya roketi vimesikika kaskazini mwa Israel asubuhi ya leo.
Vikosi vya Ulinzi vya Israel vilitoa tahadhari kwa jamii zinazozunguka mji wa Haifa na Magharibi mwa Galilaya, karibu na mpaka wa Israel na Lebanon.
Kiasi cha roketi 100 zimerushwa kaskazini mwa Israel kufikia sasa hivi, vyombo vya habari vya Israel vinaripoti, vikinukuu Jeshi la ulinzi la Israel (IDF).
Awali Jeshi la Ulinzi la Israel lilitoa tahadhari mpya kwa watu wanaoishi katika vijiji karibu vijiji 25 vya kusini mwa Lebanon wahame.
Tahadhari hii inafuatia nyingine iliyotolewa jana kwa idadi sawa ya maeneo – takriban vijiji vitano vilivyojumuishwa katika ujumbe wa hivi punde pia vilijumuishwa kwenye tahadhari ya jana.
Tahadhari hiyo kutoka kwa msemaji wa Kiarabu wa IDF Avichay Adraee, lililowekwa kwenye mitandao ya kijamii, na linakuja baada ya ripoti za mapigano kusini mwa Lebanon.
Akiwahutubia wakazi wa Lebanon walioathirika, Adraee amesema jeshi la Israel halina nia ya kuwadhuru na wanapaswa kuhama mara moja hadi kaskazini mwa Mto Awali uliopo yapata kilomita 50 kutoka mpaka na Israeli – “kuokoa maisha yako. “
Mashambulizi ya Israel dhidi ya Beirut yanatia kiwewe – Mwanasiasa wa Lebanon

Baada ya usiku mwingine wa mashambulizi ya Israel dhidi ya Beirut, mwanasiasa wa Lebanon Michel Helou ameiambia BBC kuwa mji huo una “kiwewe”.
Mbali na majeruhi, mashambulizi hayo “yanaleta wasiwasi “, katibu mkuu wa chama huru cha National Bloc nchini Lebanon amekiambia kipindi cha BBC Newsday.
“Jana usiku hakuna hata mmoja wetu aliyelala sana kwasababu ilikuwa usiku wa tano mfululizo wa mashambulizi katika kitongoji cha kusini.
“Kila saa jeshi la Israel linatuma ujumbe wa Twitter ukiwaonya watu kuhama, lakini vipi na wapi na vipi inawezekana kwao kuhama katika muda wa nusu saa kabla ya shambulio kutokea.
“Bila shaka ni jambo linalosumbua sana kisaikolojia kwa binadamu kuwa katika mashambulizi hayo.”
Mjini Beirut, Israel imekuwa ikilenga kitongoji cha kusini cha Dahieh, ngome ya Hezbollah, na inasema inachukua hatua za kupunguza hatari ya kuwadhuru raia, ikiishutumu Hezbollah kwa kuficha miundombinu yake katikati ya raia.
All Rights Reserved © Cantona Group PLC||2024
Discover more from cantonadigital
Subscribe to get the latest posts sent to your email.