Muhoozi Kainerugaba, mtoto wa kiume wa rais wa Uganda, Yoweri Museveni, ametangaza kuachana na mipango ya kuwania urais mwaka 2026, na badala yake atamuunga mkono baba yake.
Radio Fortune Africa -Na Cantona Joseph
https://zeno.fm/radio/radio-fortune-africa

Mkuu huyo wa Majeshi ya Uganda, kupitia ukurasa wake wa X ameandika kuwa, kwa sasa kazi yake kubwa ni kukiongoza kikosi cha UPDF.
Kainerugaba, ameongeza kuwa anamuunga rais Museveni ambaye hivi maajuzi alitimiza miaka 80 kuwania tena uongozi wa nchi hiyo.

Museveni ambaye amekuwa madarakani tangu mwaka 1986, hajatangaza rasmi kuwa atawania tena, lakini dalili zote zinaonesha kuwa kwa mara nyingine atapeperusha bendera ya chama tawala NRM wakati wa uchaguzi huo.
Kabla ya tangazo hili, Kainerugaba amekuwa akisema atawania uongozi wa nchi hiyo huku wachambuzi wa siasa wakisema ni wazi kuwa rais Museveni anamwandaa mwanaye ili amrithi katika miaka ijayo.

Aidha katika tangazo lake, Kainerugaba, amesema kuwa raia wa kawaida hawezi kuongoza Uganda na rais ajaye baada ya Museveni ni lazima awe mwanajeshi au polisi.
Kiongozi mkuu wa upinzani Bobi Wine, amesema ameliambia Shirika la Habari la Ufaransa AFP kuwa, hajashangazwa na tangazo la Kainerugaba kwa sababu ni wazi kuwa baba yake atawania tena urais mwaka 2026.
All Rights Reserved © Cantona Group PLC||2024
Discover more from cantonadigital
Subscribe to get the latest posts sent to your email.