Unyenyekevu ni dawa ya kufanikiwa.

Radio Fortune Africa -Inspirational Mathematics

“Angalieni mtu asiwafanye mateka kwa elimu yake ya bure na madanganyo matupu, kwa jinsi ya mapokeo ya wanadamu, kwa jinsi ya mafundisho ya awali ya ulimwengu, wala si kwa jinsi ya Kristo.”

(Wakolosai 2:8).

Kuna tofauti kati ya elimu ya Kristo na elimu ya dunia ndani ya nyumba ya Kristo.

Hizi ni elimu mbili tofauti kabisa ingawa kwa macho ya kawaida zimefanana sana, na kuna mstari mwembamba ili kuzitenganisha ambao ili kuutambua unahitaji msaada wa Mungu.

Imeandikwa katika kitabu cha Matendo ya Mitume 4:13, kwamba, “Basi walipoona ujasiri wa Petro na Yohana, na kuwajua ya kuwa ni watu wasio na elimu, wasio na maarifa, wakastaajabu, wakawatambua ya kwamba walikuwa pamoja na Yesu.

Mafarisayo na Masadukayo ambao ni wasomi na wabobevu katika mambo ya dini ya kiyahudi, waliwashangaa sana wanafunzi wa Yesu kwa ufahamu wao mkubwa juu ya mambo ya rohoni, baada ya kugundua kuwa hawajayasomea mambo hayo darasani.

Maana wanafunzi hawa walikuwa wanahubiri huku injili yao ikiambatana na dalili, ishara na nguvu za Roho Mtakatifu, lakini walipowakamata na kuwaomba vyeti vya thiolojia ndiyo wakagundua kuwa hawa watu hawajasomea thiolojia.

Siyo mbaya kusoma thiolojia ingawa matokeo ya elimu hiyo siyo makubwa katika kumdhihirisha Mungu, ukilinganisha na elimu ya kufuata kanuni za Mungu ambayo ndiyo elimu sahihi yenye matokeo katika maisha ya wokovu.

Elimu hii inajengwa katika kumuamini Mungu, na kulifanyia kazi neno lake, huku ikijumuisha juhudi binafsi katika kuutafuta uso wa Mungu, kiu ya kumtumikia Mungu, na kutamani kutumiwa na Mungu.

Hiyo ndiyo elimu inayoleta tofauti kati ya ile elimu ya dini na hiyo elimu ya rohoni.

Leo hii kuna maprofesa wa thiolojia ambao wakianza kuhubiri moyo wako unakuwa hauko connected, unajikuta unashikwa na usingizi lakini kuna vijana ambao hawajamaliza hata kusoma kitabu cha Mathayo lakini wakipata nafasi unajisikia kupokea nguvu za Mungu na majibu ya kufunguliwa na kuponywa magonjwa, hiyo ndiyo elimu ambayo ilionekana ndani ya Petro na Yohana ambayo iliwastaajabisha Mafarisayo na Masadukayo ambao walikuwa wasomi na wajuzi wa maandiko ya mapokeo ya dini.

Katika kitabu cha Marko 1:27-28, imeandikwa, Watu wote walimshangaa Yesu, hata wakaulizana, wakisema, Nini hii? Ni elimu mpya! Maana kwa uweza awaamuru hata pepo wachafu, nao wamtii!

Habari zake zikaenea mara kotekote katika nchi zote kandokando ya Galilaya.

Hii elimu iliyowashangaza ndiyo inapaswa kuwa elimu ya kwanza ambayo mkristo anapaswa kuwa nayo, maana Bwana Mkubwa alishasema kuwa alikuja duniani kwa hukumu ili vipofu waone na wanaoona wawe vipofu.

Wakati Yesu anaisema kauli hiyo, Mafarisayo ambao ni wabobevu wa elimu ya dini walitaka kufumbuliwa fumbo hilo ili wajue wao wapo katika kundi gani? La wanaona au la vipofu? Na Yesu akawajibu kuwa, “Kama mngekuwa vipofu, msingekuwa na dhambi; lakini sasa mwasema, Twaona; basi dhambi yenu inakaa.”

Habari hiyo utaipata katika kitabu cha Yohana 9 kuanzia mstari wa 39 hadi 41.

Kuona ni kujua au kuwa na elimu juu ya jambo, kwa lugha rahisi kueleweka ni kwamba Mafarisayo walikuwa na elimu ya dini ambayo imejitosheleza, na haifungui mlango wa kupokea elimu nyingine hata kama ni njema na ina uzima.

Na hii siyo dhambi ya Mafarisayo pekee bali hata wahubiri wengi sasa tumejikwaa katika hii dhambi ya kuona.

Leo hii Mungu akipitisha maonyo ya kutuonya kwa kumtumia mtoto aliyemzaa katika imani, utaona tunaanza kutazama umri wake na kuulinganisha na umri wetu katika wokovu, kisha tunamdharau na kumuweka kwenye kundi la wakosa adabu.

Tunasahau kuwa elimu ya Kristo inaambatana na unyenyekevu wa kutetemeka pale unapolisikia neno la Mungu bila kujali Mungu ameamua kulipitishia katika kinywa cha mtu wa aina gani. Maana biblia inasema, “Vinywani mwa watoto wachanga na wanyonyao Umeiweka misingi ya nguvu; Kwa sababu yao wanaoshindana nawe; Uwakomeshe adui na mijilipiza kisasi.” (Zaburi 8:2).

Kuna wakati ili tuwe salama tunapaswa kusikiliza na kuheshimu sauti hadi za watoto ambao tunadhania hawana uwezo kutumiwa na Mungu maana Mungu anaweza kuwatumia ili kupima unyenyekevu wetu.

Mimi binafsi imewahi kutokea zaidi ya mbili, mtoto wangu wa miaka minne kutumiwa na Mungu kunielekeza jambo, na kitu kilichonifanya niamini, ni ukubwa wa maneno aliyokuwa ananiambia ukilinganisha na umri wake. Na nilipothibitisha kuwa ni Mungu kamtumia tulipiga magoti na kuomba pamoja huku nikimuomba yeye ndiyo aniombee kwa Mungu.

Sisemi haya ili kujihesabia haki bali najaribu kuoanisha andiko nililonukuu na tukio halisi ambalo limewahi kunitokea.

Ukiona joho lako la udaktari wa thiolojia linakupa misimamo migumu ya kutokupiga magoti, kugalagala, kutetemeka na kulia mbele za Mungu, au linakujengea matabaka na kuchagua aina ya watu unaoweza kuwasikiliza kuhusiana na mambo ya Mungu, tambua kuwa uko kwenye kundi la wanaoona na dhambi yao inaishi.

Kuwa kipofu ni kunyenyekea na kutaka msaada wa Mungu kila wakati, hii ni pamoja na kuweka pembeni vyeti vyako, cheo chako, mali zako, heshima yako na kuikaribisha sauti ya Mungu ikuimarishe na kukupa nguvu mpya kila siku.

Watu wenye moyo huo ndiyo watu ambao Mungu huwatumia na kuwainua sana.

Tukimtazama Musa, mtumishi wa Mungu ambaye maandiko yanasema hakukuwa na Nabii kama yeye ambaye Mungu alisema nae uso kwa uso.

Huyu ni mtumishi ambaye Mungu alimpendelea na kumkabidhi muongozo wa amri kumi ambao mpaka sasa unatumiwa na imani zote kubwa zilizopo hapa duniani.

Kama hiyo haitoshi Mungu alimpa na upako wa kugawanya bahari ya shamu na ishara na maajabu mengi, lakini pamoja na hayo yote bado alikuwa mnyenyekevu, aliyeheshimu watu na akawa tayari kujifunza kwa watu kuhusu mambo mema yanayoweza kumsaidia ki huduma.

Niliposoma andiko hili katika kitabu cha Kutoka sura ya 18 mstari wa 7, niligundua kuwa mimi bado ni kipofu na ninaihitaji sana hukumu ya Mwana Kondoo inifumbue macho ili niwe mnyenyekevu.

Andiko hili linasema, “Basi Musa akatoka nje ili amlaki mkwewe, akamsujudia na kumbusu; nao wakaulizana habari; kisha wakaingia hemani.”

Yaani Musa pamoja na kuwa na heshima kubwa na kuongoza kundi kubwa la watu zaidi ya laki sita lakini bado alionyesha heshima na unyenyekevu mkubwa kwa baba mkwe wake ambaye alimuhifadhi kwa miaka arobaini kabla ya kufanikiwa.

Nikafikiria, kama mwaka 2022 ulipata gari la muujiza na likasababisha uwe mkaidi, uanze kujibizana na watu mitandaoni, ugombane na wote walioonyesha kukunipinga, vipi leo hii wewe ndiyo ungekuwa na kundi la watu laki sita?

Kwa maandishi idadi hii unaweza kuiona ndogo, lakini katika uhalisia watu hao ni wengi sana ambao wanaweza kuuharibu moyo wa mtu.

Hebu fikiria, mwaka juzi Mtume Mwamposa alijaza uwanja wa taifa ambao unaingiza watu elfu sitini, na mwaka huu pia inasemekana amekusanya watu laki mbili pale Tanganyika Perkers katika mkesha wa chako ni chako, na matukio hayo katika picha yamekuwa gumzo mitandoni na kuwa historia ya kuitikisa nchi. Sasa kwa idadi hiyo iliyowachanganya bado Mwamposa hajafikia hata robo ya kundi la watu ambao Musa aliwaongoza, lakini pamoja na ukubwa huo maandiko yanasema alipokutana na baba mkwe wake alimpokea kwa heshima kwa kumsujudia na kumbusu.

Hata Mwamposa mwenyewe ukichunguza siri ya kupata watu hao iko nyuma ya tabia yake ya unyenyekevu, nimemsikia mara kadhaa katika ibada zake akiomba Mungu ampe unyenyekevu.

Sijui kama hii umeipokea kwa mguso kama ilivyonigusa mimi ila ndani ya andiko hili kuna funzo kubwa haswa kwa viongozi kijamii (Viongozi wa dini, viongozi wa serikali, na wanasiasa).

Kama hiyo haitoshi bado Yethro alimshauri Musa jinsi ya kupanga safu ya uongozi na Musa akamsikiliza na kuupokea ushauri wake na kuufanyia kazi.

Habari hii utaisoma kwenye kitabu cha Kutoka 18:14-25

Hayo ndiyo matokeo ya elimu ya sahihi ya Mungu ambayo inampambanua mtu kwa unyenyekevu wake na heshima atakayokuwa nayo kwa watu wala siyo kwa ukubwa wa jina lake au vitu anavyovimiliki.

Ukiona elimu yako, upako, mafanikio yako, cheo chako, umaarufu wako, hekima zako, kipaji chako, au jambo lolote ambalo Mungu amekupatia halikuzalii matunda ya badiliko la tabia zako zaidi unaharibika na kuwa mtu mbaya mwenye kiburi na kuwadharau wengine, tambua kuwa bado unahitaji elimu sahihi ya Mungu ambayo ukishupaza shinngo anaweza kukufundisha kwa njia ngumu ya ugonjwa, mapigo, ugumu wa uchumi, vifungo, na jangwa ambalo unaweza kudhania ni pepo kumbe ni lugha ya Mungu ambayo itakufanya uzingatia moyoni mwako na kunyenyekea na kutambua kuwa Mungu ndiyo kila kitu, na kuheshimu watu ambao atawaleta kwako hata kama hawatakuwa na faida za moja kwa moja na wewe.

Nabii Balaamu baada ya safari yake kupingwa na Mungu, na akafumbuliwa macho na kumuona malaika, alisema maneno haya, “Asema, yeye asikiaye maneno ya Mungu, Yeye aonaye maono ya Mwenyezi, Akianguka kifudifudi, amefumbuliwa macho.” (Hesabu 24:4).

Elimu sahihi ya Mungu ndiyo inayomfumbua mtu macho, na ukifumbua jicho bila elimu hii utaendelea kuwa kipofu.

Kwa leo naomba niishie hapa, na Mungu akubariki….

All Right Reserved © Cantona Group Ltd||2024


Discover more from cantonadigital

Subscribe to get the latest posts sent to your email.

Leave a comment