UJUMBE MAALUMU KWA MITUME NA MANABII WOTE TANZANIA

Radio Fortune Africa

Kuitwa na Mungu huwa siyo jambo rahisi kama watu wengi tunavyotazamia leo.

Ndiyo maana katika maandiko, watu wengi walioitwa na Mungu hawakuitikia wito huo kirahisi bali walitoa udhuru na wengine kukimbia.

Just imagine, Yesu mwenyewe alipotaka kuwaita wanafunzi wake (Petro na Andrea) ilibidi aanze na muujuza wa kuwapa samaki nyingi (Luka 5:4-11), wala hakuwalea kwa kufunga mara kwa mara kama wanafunzi wa Yohana, ingawa alijua kabisa wakishakomaa kiimani ataondoka na yote hayo watajifunza kuyawajibikia.

Leo hii ni rahisi sana kumkosoa Yona ikiwa haujasoma historia halisi ya watu wa Ninawi, ila ukisoma vitabu na kujua sheria za watu wa Ninawi kwa wakati huo pamoja na ukatili wao kisha ukavivaa viatu vya Yona ndipo utakapopata majibu sahihi na kugundua kuwa alikuwa sahihi.

Kuwa Mtume au kuwa nabii ni kazi ngumu sana na ya hatari inayohitaji moyo wa ushujaa ili kuifanya.

Ukisoma kitabu cha Yeremia 20 mstari wa 7 hadi 14 utaona Nabii Yeremia anaomba maombi ya kulalamika hadi anailaani siku yake ya kuzaliwa na kutamani hata angefia tumboni kwa mama yake.

Maombi yote hayo ni aliomba kwasababu ya vikwazo alivyokuwa anakutana navyo katika huduma, maana watu aliotumwa kwao walimtambua kama nabii lakini hawakumuheshimu wala kuyasikiliza maneno yake.

Katika mstari huu anasema, “Nami nikisema, Sitamtaja, wala sitasema tena kwa jina lake; basi, ndipo moyoni mwangu kumekuwemo kama moto uwakao, uliofungwa ndani ya mifupa yangu, nami nimechoka kwa kustahimili, wala siwezi kujizuia.” (Yeremia 20:9).

Sentesi hii inaonyesha kuwa, kuna muda Yeremia alitamani kuachana na huduma lakini akashindwa maana wito wa Mungu kwake ulikuwa kama ndoa isiyovunjika kwa matakwa yake.

Sasa Yeremia ni mtu ambaye wito wake ulikuwa ni wa kuitwa na Mungu moja kwa moja, tofauti na sisi ambao tumemjua Mungu baada ya kuhudhulia mikutano ya injili, semina na makongamano, lakini bado mtu kama huyo anakutana na changamoto hadi anatamani kuikimbia kazi ya Mungu.

Tena bora huyo ambaye alikataliwa na kudharauliwa lakini Mungu akampa neema ya kuishi maisha marefu.

Kwenye agano tunalolitumikia (Agano Jipya) ndiyo kuna hatari zaidi, maana ukitazama wanafunzi wote wa Yesu, hakuna hata mmoja aliyeshuka kaburini kwa amani, wote walitangaza neno la Mungu kwa mateso makubwa ikiwa ni pamoja na kufungwa, kupigwa, na kufukuzwa mji kwa mji kwa ajili ya injili, lakini bado waliyavumilia yote hayo kama moja ya thawabu ya kushiriki mateso pamoja na Kristo, ambapo uvumilivu wao leo hii umetusaidia sisi kuja kumuamini Kristo katika hizi nyakati za mwisho.

Leo maandishi yao yamekusanywa na kuchapishwa na tunayanunua kama maarifa ya ki Mungu (Biblia) na yanasababisha wengine wafanikiwe kujenga majumba, kuendesha magari, kupata umaarufu, kula, kuvaa nakadhalika, na katika fahari hiyo wao wanaishia kutajwa kwa heshima ingawa wakati wanayaandika hayo walikuwa katika hofu na mashaka ya kufungwa na kuuwawa.

Hiyo ndiyo moja wapo ya sehemu ya wito wa ki Mungu ambao katika wakati wetu Mungu ametupatia nafasi ya muda mfupi wa kufurahia matunda ya injili, kupitia jasho na damu za mitume waliojenga msingi wa imani yetu kwa mateso mkubwa.

Tusipowachukua hao kama mfano wetu wa kuigwa basi tunapoelekea kuna watu wengi watageuka na kumuacha Yesu, maana zile zama za kulipa gharama kwa ajili ya kizazi kijacho zimewadia.

Tunaweza kuona kama tumefanikiwa sana na pia tumeshatengeneza mahusiano mazuri na mifumo ya dunia kulingana na majina yetu kujulikana, misaada tunayoitoa au faraja tunazopata kutoka kwa watu wanaotufurahia, bali muda siyo mrefu lugha zetu zitakwenda kubadilika na walio na wito wa Mungu kweli watajulikana.

Naliona pepeteo kubwa linakuja kwa ajili ya kuwajaribu watakatifu, ni pepeteo ambalo kila anaelitaja jina la BWANA iwe kwa mzaha au kwa uaminifu ni lazima atapimwa ndani yake, na ni wale tu wanaomtumaini Mungu kama sitara yao wakati wa shida na mateso ndiyo watakaotoka salama.

Kama wewe ni mtume au nabii kweli ingia kwenye maandalizi ya kujaribiwa kwa kuutafuta uso wa Mungu kwa bidii kubwa maana pasipo uwepo wa Mungu hakuna atakaeweza kutoka salama.

Katika kitabu cha 1 Samweli 2:9 imeandikwa hivi, “Yeye atailinda miguu ya watakatifu wake; Bali waovu watanyamazishwa gizani, Maana kwa nguvu hakuna atakaeshinda.”

UBARIKIWE SANA.


Discover more from cantonadigital

Subscribe to get the latest posts sent to your email.

Leave a comment