Hatari ya kuabudu sanamu.

Katika amri kumi za Mungu, kipengere kilichozungumzia ibada ya sanamu kinasema,

“Usijifanyie sanamu ya kuchonga, wala mfano wa kitu cho chote kilicho juu mbinguni, wala kilicho chini duniani, wala kilicho majini chini ya dunia.

Usivisujudie wala kuvitumikia; kwa kuwa mimi, Bwana, Mungu wako, ni Mungu mwenye wivu; nawapatiliza wana maovu ya baba zao, hata kizazi cha tatu na cha nne cha wanichukiao.” (Kutoka 20:4-5).

Katika kipengere hiki maandiko yameweka bayana aina moja ya kuabudu sanamu, inayohusisha kuchonga kinyago kwa kutumia mikono ya fundi, kisha kuanza kukisujudia, na kukitumikia. Lakini katika agano jipya Mtume Paulo ameenda mbali zaidi kwa kufafanua ibada hii kwamba kuna uwezekano wa kuabudu sanamu kwa njia ya mawazo binafsi pasipo kumuhusisha fundi wa kuchonga vinyago.

Amelifafanua hili katika kitabu cha Wakolosai 3:5 kwa kuandika hivi, “Basi, vifisheni viungo vyenu vilivyo katika nchi, uasherati, uchafu, tamaa mbaya, mawazo mabaya, na kutamani, ndiyo ibada ya sanamu.”

Hii aina ya pili ya kuabudu sanamu, ambayo haihusishi kuchonga taswira ya kiumbe cha aina yeyote cha mbinguni wala duniani, wala kwenye maji ndiyo mtego mkubwa unaowanasa watu wengi kwa sasa.
Japokuwa kutokana na teknolojia bado hata ile aina ya kwanza ya kuabudu sanamu inaendelea katika mtindo ambao siyo rahisi kujua kama ni ibada ya sanamu, kwa mfano kununua stika yenye picha ya nabii na kuibandika nyumbani, kwenye gari au biashara huku ukiamini kuwa picha hiyo inakulinda, kuvaa bangili za plastic zenye maandishi, au beji, kutembea na mafuta ya upako, maji ya ya upako, sabuni ya upako, asali ya upako, au kifaa chochote cha upako huku ukiamini kuwa ndiyo kinachokulinda au kukusaidia, hiyo ni ibada kamili ya sanamu.

Mara nyingi aina hii ya pili ya ibada ya sanamu inayohusisha mawazo ya mtu huwa inaanzia kwenye mtazamo wa mtu haswa atakapoweka tumaini juu ya mtu au kitu ambacho Mungu amewahi kukitumia na kikaleta majibu kwake.

Kwa muktadha huo ibada ya sanamu inaweza kuwa mtu au kitu ambacho kimewahi kukufaa na kukusaidia katika kipindi ambacho option ya mwisho ya jibu lako ilikuwa ni Mungu tu. Na Mungu akamtumia mtu au aina fulani ya kitu ambacho kitakuletea majibu.

Hivyo kumpa heshima iliyopitiliza ambayo itapelekea moyo wako kuanza kumtegemea mtu huyo au kitu hicho hiyo ndiyo inakuwa ibada ya sanamu.

Kwa mfano ametokea mtu akakusaidia ada ya mtoto au kodi ya nyumba au akakupa gari ya kutembelea, kazi au mengine mema yanayofanana na hayo, alafu kitendo chake hicho chema kikusababishe uache kuomba au kila ukiingia kwenye maombi unakuwa na picha ya mtu huyo kichwani kwa kuamini kuwa Mungu atakujibu tena kupitia mtu huyo huyo na endapo huyo mtu akikaa kimya moyo wako unaanza kuuma, unalia, na kuhisi kama maisha ndiyo yamefika mwisho, hiyo pia ni ibada ya sanamu.

Kuna wakati Nabii Samweli alitaka kuingia kwenye mtego huo wa kuabudu sanamu kwa kuamini kuwa mtu pekee mwenye uwezo wa kuongoza taifa la Israeli ni Mfalme Sauli peke yake, ndipo Mungu akamuondoa katika mtazamo huo mbaya kwa kumwambia “Hata lini utamlilia Sauli, ikiwa mimi nimemkataa asiwamiliki Israeli? Ijaze pembe yako mafuta, uende, nami nitakupeleka kwa Yese, Mbethlehemi; maana nimejipatia mfalme katika wanawe.” (1 Samweli 16:1).

Haya maelekezo ya Mungu yalikuwa ni hatua moja wapo ya kumuokoa Nabii Samweli ili moyo wake usiendelee kuchonga sanamu na kumfanya ajue kwamba Mungu ndiye mwenye watu na ana njia nyingi na pia ana watu wengi wa kuwatumia ili kutimiza makusudi yake, hivyo kumuweka mtu mmoja tu akilini mwako na kudhania kuwa bila yeye mambo hayawezi kwenda, au kuiweka njia moja na kuamini kuwa pasipo njia hiyo mambo hayawezi kwenda hiyo nayo ni ibada ya kuabadu sanamu.

Maandiko yanasema, “Mfalme Hezekia alipoanza kutawala katika taifa la Israeli, alipaondoa mahali pa juu, akazibomoa nguzo, akaikata hiyo Ashera; akaivunja vipande vipande ile nyoka ya shaba aliyoifanya Musa; maana hata siku zile wana wa Israeli walikuwa wakiifukizia uvumba; naye akaiita jina lake Nehushtani.” (2 Wafalme 18:4).

Hebu fikiria suala hili kwa upana zaidi, katika hayo yote aliyoyafanya Hezekia ambacho naamini kilizua taharuki ilikuwa ni kumvunja vipandevipande nyoka wa shaba ambaye Musa alimtengeneza kwa maelekezo maalumu kutoka kwa Mungu mwenyewe, ila kwasababu tu watu walianza kuiabudu ile sanamu ya nyoka na kuipa nafasi ya Mungu ndipo huyu mfalme akaivunja vipande vipande bila kujali ni kumbukumbu njema ya ushuhuda wa matendo makuu ambayo Mungu aliwatendea huko jangwani, lakini yeye akaivunja bila kujali watu wataona kama amemkosea heshima Musa ambaye tangu enzi za kuwakomboa watu kutoka utumwani Misri hadi leo hii bado ni kiongozi mkubwa na mwenye heshima katika taifa la Israeli, lakini Hezekia alifikia maamuzi ya kufanya hivyo ili kuwaonyesha kuwa anaestahili kuabudiwa ni Mungu pekee na siyo mtu wala kitu kinginecho hata kama aliyekitengeneza ni mtu wa heshima kiasi gani.

Leo kuna watu wanapuuza suala hili na kutengeneza mazingira ya kuabudiwa, kupigiwa magoti, kutukuzwa yaani wanaichukua nafasi ya Mungu ambaye ndiyo anaewatumia kwa ajili ya utukufu wake.

Siyo hivyo tu bali kuna ambao wengine wanazuka na mafunuo ambayo yanawasababisha watu waondoe imani yao kwa Mungu na kuelekea mifumo mingine ya kuabudu ambayo inawapelekea watu kuabudu sanamu.

Leo katika makanisa yetu kuna maneno kama papaa you are too much, go deeper na mbwembwe nyingine za kumtengenezea mazingira muhubiri au mtumishi ili aonekane kama mambo anayofanya ni uwezo wa akili zake au utaalamu wake hizo zote ni ibada za sanamu. Hata kwenye title utaona wanaandika Mtumishi fulani amponya mgonjwa wa kansa, au ampa mtoto mwanamke mgumba, yaani imefika hatua hadi kuna baadhi ya makanisa hii agenda imeshapenya kwa ukubwa kiasi kwamba hata kulitaja jina la Mungu katika matendo ya uponyaji inakuwa issue, unakuta mtumishi anataka atajwe yeye tu huku akiwahadaa watu kuwa wakimtaja yeye inatosha maana wanakuwa wameshamtaja Mungu ambaye yuko ndani yake.

Kuna wakati nilikuwa naangalia tv nikaona mtu anatoa ushuhuda wa kunusurika kwenye ajali huku akiisifia stika yenye picha ya nabii kwamba bila stika hiyo angekufa kwa ajali, na nilipojaribu kupingana na kauli hiyo wafuasi wa nabii huyo wakaniona kama muasi ninayepingana na baba yao, lakini ukweli bado unabakia pale pale kwamba ile ilikuwa ni ibada ya sanamu.

Nafasi ya Mungu iko wapi katika kanisa la karne hii? Kama inabidi tutoe pesa ili kurithishwa upako kwa jina la impartation, na kusahau kuwa Mtume Petro alimkemea vibaya Simon mchawi ambaye alitaka kupanda mbegu ili apewe nguvu za Roho Mtakatifu?!

“Hata Simoni alipoona ya kuwa watu wanapewa Roho Mtakatifu kwa kuwekewa mikono ya mitume, akataka kuwapa fedha akisema,

Nipeni na mimi uwezo huu, ili kila mtu nitakayemweka mikono yangu, apokee Roho Mtakatifu.

Lakini Petro akamwambia, Fedha yako na ipotelee mbali pamoja nawe, kwa kuwa umedhania ya kuwa karama ya Mungu yapatikana kwa mali.

Huna fungu wala huna sehemu katika jambo hili, kwa kuwa moyo wako si mnyofu mbele za Mungu.

Basi, tubu uovu wako huu, ukamwombe Bwana, ili kama yamkini, usamehewe fikira hii ya moyo wako.” (Matendo ya Mitume 8:18-22).

Je! Baba yako wa kiroho ana uwezo wa kukukemea namna hii pale unapotaka kutoa sadaka ili upate nguvu za Mungu kutoka kwake?

Wakati unaendelea kutafakari nami nitaendelea kukuletea sehemu ya pili ya somo hili…..


Discover more from cantonadigital

Subscribe to get the latest posts sent to your email.

Leave a comment