Ukosoaji wako uko vipi!!!!

Ni kipi kiko nyuma ya ukosoaji wako? Je! Unakosoa kwa lengo la kurekebisha ili kujenga? Au unakosoa kwa lengo la kuchafua ili kuharibu? Katika maswali haya mawili unapaswa kutambua kuwa, nia iliyoko nyuma ya ukosoaji wako ndiyo chombo kilichobeba agenda ya Mungu au agenda ya Shetani.

Kama kweli sisi ni wa Mungu basi nia zetu zinapaswa kubeba agenda ya kukosoa kwa lengo la kurekebisha ili kujenga, na siyo lengo la kuchafua na kuharibu juhudi na maono ya mtu maana Mungu wetu siyo muharibifu.

Nia iliyobeba agenda ya Mungu huwa inakosoa pale inapoona mapungufu na umuhimu wa kuyakosoa, lakini vilevile inapongeza pale inapoona juhudi njema za kujenga, maana huwa haibebi uadui bali inaongozwa na upendo.

Anaekukosoa pale unapokosea kwa lengo la kukurekebisha ili ufanye vizuri, huyo haupaswi kumchukia na kumchukulia kama adui, maana huyo ni rafiki mwema kwako zaidi ya mtu anaekusifia hata pale unapokosea, mwisho wa siku ukapofuka macho ya utashi wako na kuanza kushangilia maisha yako ya makosa na kuyahesabu kama sehemu sahihi ya uwajibikaji wako.

Watu wa Tiro na Sidoni baada ya kugundua kuwa Herode amewachukia waliamua kumuua kwa kumsifia hadi kwenye makosa yake na hali hiyo ikampelekea Mungu kumuua kabla ya wakati wake. (Matendo 12:20-23).

Hapa tunajifunza kuwa, kumbe njia rahisi ya kumuua mtu ni pamoja na kumpa sifa ambazo hana wala hastahili kuzipokea.

Zingatia kwamba wanaokukosoa kwa lengo la kukurekebisha na kukujenga ni marafiki wakubwa sana kwenye maisha yako hivyo unapaswa kuwapenda.


Discover more from cantonadigital

Subscribe to get the latest posts sent to your email.

Leave a comment