CantonaCast Television-Kenyan no 1 online Television Discover the Difference
Kama kawaida ya Mungu alituumba wote katika usawa, na akawekeza vitu ndani yetu, ni kweli ili tuzaliwe inahitajika wazazi wetu wakutane, mimba ipatikane, na baada ya miezi takribani tisa ndipo kiumbe azaliwe, tena wote tunazaliwa tukiwa hatuna nguo. Kinachokuja kututengeneza kuwa bora ni pale unapozaliwa na kukutana na mfumo unaokupokea duniani. Hapa ndipo tunaanza kutofautiana, mtoto aliyezaliwa mburahati kwa jongo na mtoto aliyezaliwa upanga wote hawa wanakuwa ni watoto ila status zao zinaanza kubadilika kulingana na mazingira pamoja na mifumo ya familia zilizowapokea.
Lakini pamoja na mazingira yao kuwa tofauti, ambapo mmoja anaweza kukuta ameshaandaliwa mfumo wa elimu bora, kuanzia shule chekechea mpaka chuo kikuu, lakini mwingine mfumo wa elimu ukategemea chekechea zetu za uswahilini ambazo zinakuwa mbele ya mabaraza ya nyumba za watu ambapo mwalimu anaelewa lugha ya kiswahili pamoja na ya kabila lao tu, na mtoto akimaliza hapo aingie kwenye shule za kata, bado mazingira hayo hayawezi kuondoa thamani ambayo Mungu ameiwekeza ndani ya watoto hawa, ila ili thamani ya kila mmoja ionekane ni lazima kufanya maamuzi ya kuchagua mfumo atakaosimama nao.
Thamani hailetwi na background ya familia uliyozaliwa, shule uliyosoma, wala mazingira uliyokulia ila inaletwa na maamuzi yako juu ya upande uliosimama ambao utatambulisha kipawa ambacho Mungu amekiweka ndani yako.
Ukiwa na kipawa cha uongozi lakini ukaamua kusimama vijiweni na wavuta bangi, kipawa chako kitaonekana kwao na utapata kibali hapo kijiweni, utawaongoza masela katika uharifu lakini kamwe hauwezi kuaminiwa wala kuheshimiwa kutokana na angle uliyoichagua na kuamua kuisimamia.
Leo hii tunapowaona watu mbalimbali wenye kuheshimiwa kitaifa na kimataifa, hata wengine tunashindwa kuwakaribia kutokana na ulinzi waliokuwa nao, siku ukibahatika kuonana nao utagundua kuwa ni watu wa kawaida kabisa kama mimi na wewe, ila heshima waliyo nayo imetokana na maamuzi yao ya kuchagua upande gani wasimamie ili kutambulisha vipawa ambavyo Mungu ameviweka ndani yao.
Maamuzi hayo huwa yanajumuisha kampani ya watu unaoongozana nao, mazingira utakayopatikana na mipango unayopanga juu ya maisha yako.
Ngoja nikwambie kitu ndugu yangu, leo hii Rais Magufuli angeendelea kuwa Mwalimu wa secondary huko Chato, ni dhahiri kabisa kutokana na bidii zake angekuwa mwalimu bora katika shule anayofundisha, na angepata umaarufu kwa wanafunzi anaowafundisha lakini taifa lisingejua kama kuna mwalimu bora huko Chato, ila siku alipofanya maamuzi ya kuchagua kutoka kwenye taaluma hiyo na kuamua kuingia kwenye siasa hapo ndipo mambo yalianza kubadilika hadi leo kufikia hapa alipo na kupata heshima aliyo nayo.
Heshima hii hailetwi na familia aliyozaliwa wala shule aliyosomea bali inaletwa na maamuzi aliyoyafanya ya kutafuta upande sahihi wa kusimama na kukitambulisha kipawa alicho nacho.
Kwa kusema hivi, siwashauri watu muwe wanasiasa, hapana, bali najaribu kuwahamasisha kujitathmini na kujitafakari kisha kutafuta angle ambayo inaweza kuwatambulisha na kuwapa thamani mbele ya jamii.
Leo hii tuna watu wana vitu vikubwa sana ambavyo Mungu ameviweka ndani yao, lakini vitu hivyo haviwezi kuonekana wala kutambulika kutokana na upande walioamua kusimama nao, kwa mfano kuna wanamuziki wazuri sana lakini kwa ajili ya kuendekeza stress za maisha leo hii wako mitaani wanaokota makopo na vyuma chakavu, na wakishapata chochote wanakimbilia kirabuni kunywa chang’aa na kisha wanaimba na kufurahi kisha wanarudi nyumbani kulala. Camon, ukiitambua thamani yako utachagua hata maeneo ya kunywea kinywaji chako pamoja na kampani mtakaokuwa mnakunywa nao.
Thamani ya mtu inatokana na maamuzi binafsi na siku zote Mungu huwa anazitia nguvu hatua za mtu anaeamua kuchukua maamuzi yenye maana katika maisha yake.
Unapochukua maamuzi ya kuitambulisha thamani yako wapo watakaosema una dharau, unawatenga, wengine watakupinga, watajaribu kukuzuia hata kukuua lakini wewe usisimamishwe na hizo changamoto, you just go.
Andika barua ikulu, mwambie rais nataka uwe rafiki yangu, kaa na wabunge, viongozi wakubwa, wanamuziki wenye akili, wataalamu wa mambo mbalimbali, wafanya biashara, hata kama itakughalimu kujipendekeza wewe jipendekeze tu maana zote hizo ni gharama za kutafuta kuutambulisha uthamani wako mbele ya jamii.
Siyo kila siku umekaa na watu wale wale, maeneo yale yale, mnalalamika tu maisha yalivyo magumu, no, badilisha mazingira, badilisha marafiki, pambania thamani yako kwa kufanya maamuzi huku ukimtanguliza Mungu.
Mungu siku zote huwa yuko upande wa watu wanaopambana ili kutambulisha ubora wao na sio wale waliokaa chini ili kungoja siku moja atelemke kutoka mbinguni na kuwapatia kile wanachohitaji, so just stand up and fight for what you believe….
Discover more from cantonadigital
Subscribe to get the latest posts sent to your email.