Spana ya ubongo wa Imani ya mkristo.

CantonaCast Television- No 1 Online Television Discover the Difference.

“Na Mungu, je! Hatawapatia haki wateule wake wanaomlilia mchana na usiku, naye ni mvumilivu kwao?
Nawaambia, atawapatia haki upesi; walakini, atakapokuja Mwana wa Adamu, je! Ataiona imani duniani?”
(Luka 8:18).

Haya ni maneno ya Yesu Kristo kabla ya kusalitiwa, kisha kusulubiwa, kufa, na siku ya tatu kufufuka na kupaa kwenda kuketi kuume kwa Mungu baba juu mbinguni.
Aliongea juu ya haki, kwamba kilio cha mteule wake juu ya haki akilia mchana na usiku Mungu atampatia hiyo haki, ama kwa lugha nyepesi ni kwamba Mungu ataendelea kujibu maombi ya watu wake wanaomlilia usiku na mchana.

Katika hili tunaona Yesu akiwa hana mashaka na maombi yetu kujibiwa, lakini swali la Yesu linakuja kuonyesha mashaka juu ya imani anayoiacha kwa watu kama watastahimili kuienzi hadi siku atakayorudi duniani.
Je! Atakaporudi kulichukua kanisa ataikuta imani hiyo bado ipo au atakuta tayari imani imeshapotea na watu wamegeukia imani zingine?
Haya mashaka ndani ya swali hilo yanaonyesha kuwa jicho la kinabii la Yesu lilitazama kwa umbali mrefu hadi katika karne hii ya ishirini na moja, miaka hii ya leo (miaka elfu mbili na ishirini baada ya kifo chake) na kuona jinsi sisi wakristo ambao ndiyo wafuasi wake namba moja tutakuja kugeukia imani nyingine ambazo zinapingana kabisa na mafundisho yake badala ya kuishi kile alichotufundisha.

Katika msingi wa imani aliyoifundisha Yesu kitu kikubwa alitufundisha ni upole na unyenyekevu (Mathayo11:29), lakini leo hii kanisa limekosa watu wapole na viongozi wake sio wanyenyekevu, wanajiita mababa wa kiroho wakati Yesu alishasema tusimuite mtu baba duniani (Mathayo 23:9).

Katika msingi wa imani aliyoifundisha Yesu alisema kwa jina lake tukiomba chochote tutajibiwa (Yohana 14:13-14), lakini leo asilimia kubwa ya watumishi wake hatulitumii tena jina lake bali tunawaombea watu kwa majina yetu wenyewe (Kwa jina la Mungu wa Bashando) huku tukiwaaminisha kwenye vitu kama vile maji, chumvi, mafuta, keki, stika, vitambaa nk.

Katika imani aliyoifundisha Yesu aliwahi kuwakataa watu waliomfuata kwa ajili ya kutaka miujiza tu na wala siyo kwa ajili ya kuliamini neno la Mungu na akawaambia wasikitendee kazi chakula kinachoharibika, bali chakula kidumucho hadi uzima wa milele (Yaani neno la Mungu, Yohana 6:25:29), lakini leo hii sisi tunawaita watu wanaotaka miujiza tu na kuwahakikishia kuwa watapokea kile wanachokihitaji (ndoa, magari, kujenga nyumba, kusafisha nyota ya biashara, safari za ulaya nk) na mbaya zaidi wakija katika makusanyiko yetu hatuwafundishi kwa malengo ya kuwafanya wanafunzi wa Kristo bali tunawatengeneza kuwa followers wetu huku tukiwapora pesa zao kwa njia za ujanja ujanja.
Katika imani aliyoifundisha Yesu alikuwa anakataa kabisa kuuchukua utukufu wa Mungu hata katika maneno ambayo mtu anamtamkia (Luka 18:19), lakini leo sisi watumishi wake tunaruhusu watu watupigie magoti hata kutusujudia kwa kigezo kwamba tumembeba Yesu ndani yetu na wanavyosujudu au kupiga magoti huwa wanaiheshimu neema iliyoko ndani yetu.
Hebu tuwatazame hawa wafuasi wa kweli wa Kristo jinsi walivyokabiliana na kiburi cha uzima ili kupitia wao tuweze kufunguka macho na kugundua kuwa tumepishana mbali sana na ile imani aliyotuachia Bwana na mwokozi wetu Yesu Kristo….
Biblia inasema, “Na makutano walipoona aliyoyafanya Paulo wakapaza sauti zao, wakisema kwa Kilikaonia, Miungu wametushukia kwa mifano ya wanadamu.
Wakamwita Barnaba, Zeu, na Paulo, Herme, kwa sababu ndiye aliyekuwa mnenaji.
Kuhani wa Zeu ambaye hekalu lake lilikuwa mbele ya mji, akaleta ng’ombe na taji za maua hata malangoni, akitaka kutoa dhabihu pamoja na makutano.
Walakini mitume Barnaba na Paulo, walipopata habari, wakararua nguo zao, wakaenda mbio wakaingia katika makutano, wakipiga kelele,
wakisema, Akina bwana, mbona mnafanya haya? Sisi nasi tu wanadamu hali moja na ninyi; twawahubiri habari njema, ili mgeuke na kuyaacha mambo haya ya ubatili na kumwelekea Mungu aliye hai, aliyeumba mbingu na nchi na bahari na vitu vyote vilivyomo” (Matendo 14:11-15).
Hawa mitume na manabii wa kweli waliozifuata nyendo za Kristo kwa kukataa kabisa kuchukua utukufu wa Mungu wa kukubali kutolewa sadaka, licha ya kufanya ishara kubwa zilizobadilisha akili na mitazamo ya watu wa jamii yao, lakini mitume na manabii wetu leo ukiwaona wanaingia kanisani au wanapita mbele yako inabidi utoe sadaka ya kujiungamanisha na upako wao (Kujikonekti).
Namaliza kwa kukuuliza swali alilouliza Bwana na mwokozi wetu Yesu Kristo, Je! Siku akirudi kukuchukua ataikuta imani?


Discover more from cantonadigital

Subscribe to get the latest posts sent to your email.

Leave a comment