Nguvu pamoja na hukumu ya shahidi.

Katika maisha shahidi huwa ni mtu wa muhimu sana katika kuongeza nguvu juu ya kitu kile ambacho watu wanakiamini.
Haijalishi ni maisha ya imani, au katika mchakato wa kutafuta haki….

Biblia inasema, “Nao wakamshinda kwa damu ya Mwana-Kondoo, na kwa neno la ushuhuda wao; ambao hawakupenda maisha yao hata kufa” (Ufunuo 12:11). Unaona hapa ushuhuda unatamkwa kama sehemu ambayo iliwasababishia watu ushindi. Yaani pamoja na kuomba kwa kutumia damu ya mwanakondoo (Yesu) lakini bado walitumia ushuhuda wao ili kutafuta ushindi na wakafanikiwa kushinda.

Hata mahakamani ushahidi ndiyo huwa na nguvu ya kusababisha hakimu atoe hukumu ya haki ambayo haitaonea pande zote mbili (mshataki/mshatakiwa).

Ukiitwa polisi kama shahidi ili kutoa ushahidi katika kusaini fomu ile ya shahidi kuna kipengere kimeandikwa kuwa “Endapo ukibainika umetoa ushahidi wa uongo uwe tayari kuhukumiwa kifungo kwa mujibu wa sheria.”

Hii inaonyesha ni jinsi gani ushahidi una nguvu katika kutengeneza kesi kiasi kwamba mtu akitumika kama shahidi wa uongo katika kesi yeyote basi anapaswa hukumu.

Moja ya maagizo ambayo Mungu alimuaguza Musa awaambie wana wa Israeli wakati wako jangwani ni hii, “Usivumishe habari za uongo; usitie mkono wako pamoja na mwovu, kuwa shahidi wa udhalimu.
Usiandamane na mkutano kutenda uovu; wala usitie ushahidi wako katika neno lo lote kwa kugeukia kando na kuandamana na mkutano ili kupotoa hukumu” (Kutoka 23:1-2). Hata katika amri zake kumi Jehovah alitoa amri inayosema, “Usimshuhudie jirani yako uongo” (Kutoka 20:16).

Hizi ni amri na maagizo ya Mungu mwenyewe yanayokataza watu wake kutoa ushahidi wa uongo kwa namna yeyote ile.

Katika kipindi tulichopo hii dhambi ya kushuhudia uongo inapaswa kukemewa sana kwa sababu watu wengi wanaitenda bila kujua kama hiyo pia ni dhambi.

Wewe ambaye umewahi kushuhudia uongo iwe polisi, mahakamani, au kanisani unapaswa kujua kuwa mbele za Mungu hiyo ni dhambi kubwa.

Leo kuna watu wanalipwa na wachungaji, mitume, manabii, maaskofu kwa ajili ya kutoa ushuhuda wa uongo madhabahuni, unakuta mtu anajidai kama alikuwa kichaa, au amelala kwenye kitanda kama mgonjwa mahututi, wengine wanapakwa majivu na masizi usoni kisha wanaigiza kama misukule, wengine wanapiga simu redioni na kushuhudia kama walikuwa wanaumwa na sasa wamepona, wengine wanaigiza kama wachawi waliondondoka nje ya kanisa kwa kuzidiwa na nguvu za Mungu. Hayo yote wanayafanya kwa ajili ya kumpa heshima mtumishi wa kanisa husika na siyo kumpa heshima Mungu.

Haya yote mbele za Mungu ni machukizo na yeyote utakaehusika au ambaye umewahi kuhusika kufanya ulaghai wa aina hii unapaswa kutubu na kuacha mara moja.

Mungu wetu amekataza ushuhuda wa uongo kwa sababu ushuhuda wa uongo hauwezi kubeba utukufu wake bali utabeba maslahi ya mtu binafsi, maana yote hayo ambayo mtu anaweza kutumika ili kudanganya, Mungu ana uwezo wa kuyafanya hata makubwa zaidi bila kutumia njia za uongo.

Inasikitisha sana matukio haya ya uongo yanazidi kushika kasi huku wahusika wakiyapachika jina la nyoka ya shaba huku wakijifariji kuwa, kama Musa alitengeneza nyoka wa bandia ili kuwaponya wana wa Israeli na nyoka wa moto hivyo na wao wana haki ya kutengeneza miujiza na shuhuda feki ili kuinua imani za washirika wao.
Uongo wowote Mungu wetu hawezi kuuridhia kwa sababu Yesu alishasema kuwa, shetani ndiyo muongo na baba wa huo na kila anaedanganya huyo ni mtoto wa shetani, (Yohana 8:44).

Hakuna haja ya kupandikiza hirizi kwenye nyumba za washirika wenu wenye uwezo kifedha na kuwadanganya kuwa wamerogwa kisha kuwaomba sadaka za ukombozi. Hizo njaa zenu za kutaka mafanikio ya haraka haraka yanalidhalilisha kanisa, na biblia inasema, “Utajiri na heshima ziko kwangu, Naam, utajiri udumuo, na haki pia.” (Mithali 8:18). Tukimlingana Mungu sawasawa vyote tutavipata kwake kwa njia iliyo halali wala siyo kwa udanganyifu.

Hebu tuache uvivu wa kuomba na tubadilishe mfumo wa maisha kwa kukubali kulipa gharama. Badala ya kukutana kwenye migahawa na kunywa juice huku tukupiga stori za kutafuta pesa kwa matajiri, wanasiasa pamoja na viongozi wa serikalini sasa tuanze kukutana milimani kwenye maombi ili kutafuta nguvu za Mungu, na hapo ndipo miujiza halali itaanza kutokea kwenye huduma na makanisa yetu na nguvu ya kanisa itaendelea kushika hatamu.

Mungu akubariki na akusaidie kuuelewa ujumbe huu… Kama umekugusa tubu mara moja na uache njia mbaya, lakini pia unaweza ku share kwa wengine pia ili maonyo haya yaweze kuwafikia wengi….


Discover more from cantonadigital

Subscribe to get the latest posts sent to your email.

Leave a comment