Manabii was uongo katika kizazi hiki

Kwa kweli huduma ya kinabii imevamiwa na wapunga pepo ambao kwa asilimia kubwa ndiyo wanaoharibu sura ya kanisa haswa kwa bara letu la Afrika.

Wamefanya injili ya sasa imekuwa ni injili ya tofauti kabisa na ile aliyoihubiri Bwana na mwokozi wetu Yesu Kristo.
Sasa hivi manabii wa uongo wanatumia muda mwingi sana kutuhubiria juu ya injili ya mafanikio huku wakitujengea chuki kwa kutengeneza uadui kati yetu ambao hauna manufaa kabisa katika ufalme wa Mungu.
Utasikia wanafundisha kuwa, “adui zako wanakwenda kuaibika, waliokuroga usifanikiwe wanakwenda kufa, waliokudharau wanakwenda kukupigia magoti”. Na washirika wao wanaitikia kwa furaha amen, I receive, go deeper papaa… Wanashindwa kuelewa kuwa Yesu alishatuagiza kuwapenda maadui zetu (Mathayo 5:44), na pia maandiko yanatusisitiza tusiwalaani wanaotuudhi bali tuwabariki (Warumi 12:14). Na huu ni mfumo uliokuwepo tangu zamani ambapo maandiko yatuelekeza kwamba, “Adui yako akiwa ana njaa, mpe chakula; Tena akiwa ana kiu, mpe maji ya kunywa; Maana utatia makaa ya moto kichwani pake; Na Bwana atakupa thawabu” (Mithali 25:21-22). Kumbe njia sahihi ya kumshinda adui yako na kupata thawabu kwa Mungu siyo kumuua katika maombi bali ni kumtendea wema.

Sasa hii injili ya manabii wengi wa uongo siyo injili sahihi maana inapingana na mfumo wa utendaji kazi wa Mungu, kwa kweli hii ni injili ya aina nyingine ambayo Paulo alipoiona kwa Wagalatia aliwaambia, “Nastaajabu kwa kuwa mnamwacha upesi hivi yeye aliyewaita katika neema ya Kristo, na kugeukia injili ya namna nyingine. Wala si nyingine; lakini wapo watu wawataabishao na kutaka kuigeuza injili ya Kristo.” (Wagalatia 1:6-7). Hao watu ambao walikuwa wanawataabisha Wagalatia enzi hizo, naamini kwa sasa ndiyo hawa wanaojiita manabii. Maana injili ya manabii wa sasa imeua upendo kabisa ndani ya kanisa na kusababisha watu wawe na akili za kishirikina na kuanza wanaomba maombi ya kulaaniana na kunyongana wenyewe kwa wenyewe. Injili hii imewageuza washirika wengi wa manabii kuwa washirikina wa kifikra, yaani mtu anawazia kurogwa na kukwamishwa wakati neno la Mungu linasema, “Hakuna uchawi juu ya Yakobo wala hakuna uganga juu ya Israeli” (Hesabu 23:23). Ukimuishi Mungu sawa sawa na kushika amri zake hakuna mchawi atakayekuroga. Balamu alitaka kuwaroga wana wa Israeli lakini mwisho wa siku akajikuta anawabariki kwa sababu hawarogeki, wanalindwa na nguvu za Mungu.
Unakuta nabii mwingine anamtabiria mtu kuwa amerogwa na mume wake au shangazi yake au ndugu za mume, na kujikuta ametengeneza mfarakano kwa kupandikiza fitina katika familia, kibiblia hili ni kosa na tena ni chukizo mbele za Mungu (Mithali 6:19). Lakini pia hii ni ramli chonganishi na iko kinyume hata na sheria za nchi ya Tanzania.
Hivyo nyie manabii mnapoelekea ule utabiri wa Askofu Kakobe juu yenu wa nyinyi kufungwa pingu unaenda kutimia, maana mnamkosea Mungu, mnalidhalilisha kanisa, na pia mnakiuka sheria na taratibu za nchi.
Uhuru wa kuabudu usiwe sababu ya kutenda mabaya kwa kivuli cha imani. Msipobadilika unakuja wakati ambao maneno yangu haya mtayakumbuka huku mkiwa mmefungwa magerezani, maana hukumu ya Mungu ipo karibu kuanza.
TUBUNI KWA MAANA UFALME WA MUNGU UMEKARIBIA.


Discover more from cantonadigital

Subscribe to get the latest posts sent to your email.

Leave a comment