NJIA YA MKATO SIYO NJIA SAHIHI KATIKA MAISHA.
Katika mahubiri ya ibada ya kila usiku hapa nyumbani nimesoma andiko kutoka katika kitabu cha Mithali 3:5-9.
Sikuwa nimeandaa mahubiri ila namshukuru Mungu kwa kuwa injili ya leo imenifundisha zaidi, na ninadhani mimi ndiyo nimepokea zaidi ya niliyokuwa nawahubiria.
Katika andiko hilo, neno la Mungu linasema, “Mtumaini Bwana kwa moyo wako wote; wala usizitegemee akili zako”
Nikajifunza hapa kuwa mfumo wa mafanikio ya mwanadamu upo katika kumtumaini Mungu na kumtegemea kwa moyo wake wote.
Mungu ametupa akili ili tuzitumie ila siyo tuzitegemee, maana short cut way ni mfumo wa mtu anaetegemea akili na kuacha kumtumaini Mungu.
Wakati Daudi amekimbia ikulu ya Israeli kwa hofu ya kuuwawa na mfalme Sauli, akili yake ilikuwa imeshajengeka katika maisha ya kiwango cha ufalme, hivyo moja kwa moja alikimbilia katika nchi ya Gathi kwa mfalme Akishi ili kupata hifadhi (1 Samweli 21:10).
Hapo alikuwa mkimbizi wa kisiasa ambaye ameshapoteza haki zake zote za kazi ikiwemo kiinua mgongo katika kazi yake ya jeshi la Israeli alilokuwa amelitumikia kwa miaka kadhaa.
Hivyo katika sakata hili Daudi alikuwa na hofu za aina mbili..
▪Hofu ya kutafutwa kuuwawa na mfalme.
▪Hofu ya kuanza moja baada ya kupoteza ajira
Katika hofu na mashaka hayo alijikuta anachukua maamuzi yasiyo sahihi kwa kutafuta msaada na huruma za wanadamu badala ya kumtegemea Mungu.
Mpango wake huo uligonga mwamba baada ya baadhi ya maafisa usalama (Mashushu) wa nchi ya Ghati kumshtukia kama yeye ni mmoja wa maaskari wa Israeli ambao wako katika rank ya juu ya kukaa na mfalme, hivyo ili kukwepa msala huo ikabidi ajidai kama amechanganyikiwa na kukimbilia pango la Adulamu.
Kwa taratibu za kijeshi inahesabika kama Daudi aliponea chupu chupu kuwekwa kizuizini au kuuwawa kama mpelelezi aliyepenya ili kuipeleleza nchi hiyo, maana kila askari katika kila nchi hawezi kuruhusiwa kwenda mkoa mwingine ama nchi nyingine bila barua ya ruhusa (movement order).
Hivyo basi Daudi kusalimika na kutoka salama mbele ya mfalme wa Ghati ilikuwa ni kama bahati ya ngekewa kwa sababu ilikuwa ni kosa katika sheria za kijeshi.
Akiwa katika pango la Adulamu huku hana hata pa kuanzia, na bado yuko katika hali ya uchungu wa kupoteza ajira, hofu juu ya Sauli, pamoja na kunusurika kifo au kifungo cha kijeshi mbele ya mfalme wa Gathi, tunaona Daudi anafuatwa na watu waliochoka ambao hawawezi kumsaidia chochote.
Biblia inasema, “Alifuatwa na watu wenye madeni na wenye uchungu nafsini kwao na kumfanya awe jemedali wao (1 Samweli 22:2).
Huu wote ulikuwa ni mchakato wa Mungu kumtengeneza moyo wake ili aweze kumtumaini Mungu na kuacha kabisa kuzitegemea akili zake.
Watu wengi leo wanatamani kuwa kama Daudi ila hawajawahi kutafakari jinsi Mungu alivyomuandaa katika njia za mateso ili kumfanya awe kama vile alivyo.
Katika Zaburi 118:8-9, Daudi anasema, “Ni heri kumkimbilia BWANA kuliko kuwatumainia wanadamu. Ni heri kumkimbilia BWANA kuliko kuwatumainia wakuu”. Mambo haya hakuyaimba ili mradi tu, bali ni kwa sababu alikuwa na uzoefu wa kutosha juu ya hali mbalimbali katika maisha yake.
Kuna wakati Mungu anaruhusu tupitie magumu, kukataliwa, kuchukiwa, kupingwa na watu tunaodhania kuwa wanatufaa katika dhiki zetu, na pia kutuletea watu ambao kwa wakati huo hawana msaada wowote zaidi ya kututegemea, lakini yote haya anayafanya ili kutufundisha kutoishi kwa kutegemea akili zetu bali kumtumaini yeye katika hali zote.
Kama umebarikiwa na fundisho hili unaruhusiwa kushare na wengine ili waipate elimu hii.
Discover more from cantonadigital
Subscribe to get the latest posts sent to your email.