Ole wangu masikini

🎚️Warumi 7 Katika aya ya 15-25 Paulo anaeleza uhalisi wa hali yetu ya dhambi. Dhambi ambayo ni uasi wa sheria, ni tendo hasa la rohoni kama ilivyo sheria yenyewe. Lakini matokeo yake huonekana kwa nje. Paulo anaonyesha jinsi asili ya dhambi ilivyofungamana nasi katika hali ya anguko.

🎚️Dhambi imo ndani yetu, ni hali yetu, ni asili yetu, Naam ni sheria iliyo katika viungo vyetu na inatawala utendaji wetu. Na kwa kujitambua kuwa hawezi kujiokoa mwenyewe dhidi ya mwili huu, Paulo anasema “Ole wangu masikini mimi ni nani atakayeniokoa na mwili huu wa mauti”? Hii ni hali ya kila mtu nje ya Kristo. Tuu masikini tusioweza kujiokoa wenyewe.

🎚️Lakini Mungu ashukuriwe kwa kumtoa mwana wake ili kutukomboa. Ni katika Kristo Yesu peke yake ushindi dhidi ya dhambi unapatikana. Paulo anahitimisha kwa kumshukuru Mungu kwa kipawa chake Anasema “Namshukuru Mungu kwa Yesu Kristo Bwana wetu….”kwa hiyo tumaini letu pekee la wokovu dhidi ya mwili huu wa mauti kama ilivyokuwa kwa Paulo ni BWANA MWOKOZI WETU YESU KRISTO. Kwa neema ya Mungu hebu tufungue mioyo yetu sasa na kumpokea Roho Mtakatifu ili akae ndani yetu na kutawala maisha yetu milele zoye. Haleluya!

🎚️Katika Warumi 8:1-17 Mtu anapokuwa amempokea Yesu Kristo kuwa Bwana na mwokozi wake, basi hakuna tena hukumu ya adhabu juu yake. Hii ni kwasababu Kristo aliye ndani yake ametimiza madai yote ya torati ya Mungu na hivyo haki ya Kristo inahesabiwa kuwa yake na anapatiwa Haki hiyo moyoni na anavikwa haki hiyo.

🎚️Halipwi mshahara wa dhambi ambao ni mauti bali anapewa kile ambacho ni stahili ya Kristo yaani uzima wa milele. Sasa yuko huru katika Kristo kwa njia ya sheria ya Roho wa uzima ulio katika Kristo Yesu.

🎚️Bwana anachukua dhambi ya mtu aliyetubu na kumpatia haki yake (Tabia yake) anamvua nguo chafu (yaani matendo maovu) na anamvika vazi la haki yake – Zekaria 3:1-5 Hivyo anaposimama mbele za Mungu, anasimama akiwa amevikwa Haki ya Kristo iliyochukua pahali pa dhambi zake.

🎚️Sheria ya roho wa uzima ni ile sheria takatifu ya Mungu iliyo ya uhuru Yakobo 2:12 ( Semeni ninyi, na kutenda kama watu watakaohukumiwa kwa sheria ya uhuru) Lakini sheria ya dhambi na mauti ni ile nia ya mwili inayotuongoza kutenda maovu -Rum 7:10,23,24; 8:6,7 Kumfuata Yesu ni kuifia nafsi kujikana nafsi kwaajili yake na kuruhusu mapenzi yake yatimizwe ndani yako.


Discover more from cantonadigital

Subscribe to get the latest posts sent to your email.

Leave a comment