Neno la leo

1 Timotheo 1: 18 – 20

“Mwanangu Timotheo, nakukabidhi agizo hilo liwe akiba, kwa ajili ya maneno ya unabii yaliyotangulia juu yako, ili katika hayo uvipige vile vita vizuri; uwe mwenye imani na dhamiri njema, ambayo wengine wameisukumia mbali, wakaangamia kwa habari ya Imani. Katika hao wamo Himenayo na Iskanda, ambao nimempa Shetani watu hao, ili wafundishwe wasimtukane Mungu.”

Mtume Paulo anamuandikia Timotheo ambaye ni mwanaye katika Imani, akimkumbusha juu ya wajibu aliomwachia wa kulichunga kanisa pale Efeso, katika kipindi ambacho kulikuwa na changamoto ya mafundisho potofu.

Pamoja na kwamba Injili ya Kristo ilihubiriwa na watu wakamwamini Yesu, walikuwepo wapotoshaji waliokaza juu ya sheria na taratibu ambazo kwa hizo waliwachanganya waumini.

Mtume Paulo anawaita ni walimu wa uongo, na hapa amewataja Iskanda na Himenayo. Hivyo anamtahadharisha Timotheo kujiepusha nao na pia alisaidie kanisa lisipotoshwe.

Mpendwa, changamoto ya upotoshaji katika kanisa bado ni kubwa hata leo. Siku hizi tunashuhudia mikazo mingi ya mafundisho yanayoisukumia mbali neema ya Mungu kwa watu kukaririshwa kufanya mambo fulani ili wakamilike katika mahusiano na Mungu.

Wakati mwingine nathubutu kusems ushirikina umeingizwa kanisani kwa namna nyingi, na waumini wamechanganywa.

Watu wanaishi kwa hofu kubwa maana mafundisho juu ya majini, mapepo, freemasoni, uwezo na nguvu ya shetani vimehubiriwa zaidi kuliko uwezo na nguvu Ukombozi wa Yesu Kristo.

Mikazo ya matambiko ya Agano la kale juu ya ukombozi imepata nafasi kuliko kazi ya msalaba aliyoifanya Kristo.

Ikumbukwe kwamba nia ya wapotoshaji hawa ni kujitafutia mali na mafanikio ya haraka.

Mpendwa, ni wakati wa kuwa makini na upotoshaji unaoendelea, tuishike Imani ya kweli katika Kristo Yesu.

MUNGU AKUBARIKI


Discover more from cantonadigital

Subscribe to get the latest posts sent to your email.

Leave a comment