Kesheni mukiomba.

MAOMBI YA USIKU WA MANANE NA ALFAJIRI.

KUEPUKA MATESO KWA SABABU YA MAAMUZI YA ZAMANI .

▪Kuna watu wako katika maisha magumu kiuchumi, kiroho , kiakili, kihisia na katika maeneo mengi kwasababu ya maamuzi waliyofanya zamani.Kuna maamuzi ambayo bado yanawaathiri watu hata baada ya kuamua kuokoka. Ni kwasababu bado hawajajua kwamba ukiokoka mambo yote yanakuwa mapya katika ROHO.Lakini upya huu lazima uletwe katika nafsi mpaka akili isome maisha mapya ndani ya Kristo na mwili ufahamu hilo.

▪ Wala msiifuatishe namna ya dunia hii; bali mgeuzwe kwa kufanywa upya nia zenu, mpate kujua hakika mapenzi ya Mungu yaliyo mema, ya kumpendeza, na ukamilifu.[ Warumi 12:2]
Kuna nguvu ya kuifuatisha namna ya ulimwengu huu ndani ya mwamini.Kuna ile nguvu inakuvuta kuishi maisha ya zamani.Ndio maana unajua kabisa umeokoka lakini bado unasikia hamu ya pombe na uasherati, unasikia hamu ya kuiba na unadanganya bado . Unajitahidi kujizuia lakini kuna namna unashindwa na kuanguka tena na tena. Maisha yako yamejaa hukumu na majuto kwasababu unayofanya hutaki kuyafanya.

▪ Wengine sio katika matendo mabaya. Lakini kuna maamuzi fulani umefanya yanakuathiri mpaka leo. Ukikumbuka ni maumivu. Unakumbuka namna ulivyokataa shule. Wengine walipata fulsa ya kuolewa na watu wacha Mungu lakini wakawakataa na kuwafuata watu wengine na leo wako kwenye mdoa chungu mno.Mwingine aliwahi kutendewa kitu cha kuumiza na mpaka leo yuko kwenye maumivu ameshindwa kusamehe adui anatumia leo hii hali ya kutosamehe kumuumiza leo. Mambo hayaendi kwasababu hajasamehe.Wengine wako kwenye ndoa lakini hawana radha na maisha ya ndoa kuna hali ya kuwakumbuka wapenzi wao wa zamani na wanawalinganisha na wake au waume zao. Pengine walifanya uasherati na wapenzi wale na sasa hawapati yale walipata huko kabla ya ndoa. Inawatesa sana.

▪ Kuna mambo mengine wengine walipokea matatizo walipokaribisha watu wasiofaa kwenye familia zao. Wengine walikaribisha ndugu na marafiki na hawa ndugu na marafiki wakatembea na wake zao au waume zao.Hii imewatesa mpaka leo.Mwingine alikosea kitu fulani na kipo akilini mpaka sasa. Kila akisogea mbele za Mungu kuomba akili inaenda kule kumkumbusha lile jambo. Analiona kila akipiga magoti kuomba na linamtesa na kumuumiza.
Wengine wakiwa vijana walifanya michezo ya punyeto wakaamini wakioa au kuolewa wataacha. Sasa wameoa na kuoelewa lakini hali hii bado inaendelea hawawezi kabisa kupona kutoka katika matatizo haya.Na yanavuruga kabisa akili zao, adui anatumia kama mlango kutesa fikra zao na maisha yao ya furaha, uchumi unayumba kwasababu ya mambo ya zamani.

▪ Kuna makosa wengine walifanya wakiwa hawajui na sio kwamba wanayakumbuka na hata wakikumbuka bado fahamu zao za kawaida hazieelewi kwamba ni makosa. Wengine walikwenda mahali ambako hawakutakiwa kwenda, walisoma masomo ambayo hawakutakiwa kusoma na sasa wanafanya kazi ambazo hata hawana furaha nazo.Hawaelewi shida iko wapi? Mbona wanajitahidi lakini mambo hayaendi? Kuna wengine wanateseka na maamuzi yao ya kuolewa na kuoa watu fulani. Kusafiri kwenda nje kufanya kazi au masomo, kuna watu wamekosea mahali fulani aidha kwa kujua au kutojua na mpaka sasa imekuwa mateso.

▪ Kuna madhabahu imejengwa kwenye akili ya watu kadhaa. Toka siku alipodanganya kwenye mahusiano akiwa chuo na kuwa na wanaume wawili mpaka leo kaolewa au kuoa na hawezi tena kutulia. Hata kama hana mtu bado anasikia kutamani kuwa na mtu mwingine tena na hajui sababu.
Nataka nikwambie kwamba hayo yote yanawezekana kuondoka ukiomba leo kwa imani. Jitazame na uone maisha unayoishi yameathiriwa na kitu gani? Anza kumwambia Mungu akushughulikie na kukusaidia kushinda. Amua kuoana kwamba mambo ya zamani ni ya zamani. Mwambie Mungu ayaondoe akilini mwako na kukutakasa kabisa. Akufanye kuwa msafi na uanze maisha mapya. Kama unajitaji kusamehe mwambie Mungu akupe nguvu ya msamaha na uamue kusamehe usijizuie kusonga mbele. Kama uliumizwa kwenye mahusiano basi achia moyo wako katika bahari ya msamaha na usonge mbele.

▪Nanyi kama mkiona ni vibaya kumtumikia BWANA, chagueni hivi leo mtakayemtumikia; kwamba ni miungu ile ambayo baba zenu waliitumikia ng’ambo ya Mto, au kwamba ni miungu ya wale Waamori ambao mnakaa katika nchi yao; lakini mimi na nyumba yangu tutamtumikia BWANA. [Yoshua 24:15]

Wengine maamuzi ya wazazi wetu, mababu na mababu yalikuwa ni kutumikia miungu mingine. Na wakafanya matambiko, wakatoa kafara na kuweka maagano. Ndio maana leo kuna athari kwenye maisha yako. Ni kweli roho yako imeokoka na ukifa utaenda mbinguni. Lakini tayari umeshazaa na wanaume watatu mpaka sasa na hata huelewi nini kilitokea. Kila mahusiano yanavurugika.

▪ Huyu ni Farao anaendelea kukufuatilia na kukutisha akutese.Anajua kabisa Mungu alishamtuma Yesu kukukomboa wewe na kila ulichonacho lakini bado anakufuatilia.Leo nataka ukatae hii hali . Mwambie Mungu aondoe athari zote za maamuzi yako aua ya wazee wako ambayo yanakuumiza leo na kukutesa.

MAOMBI.

¤ BWANA MUNGU ahsante kwa ajili ya usiku huu. Nakuomba siku ya leo unipe nafasi ya kuanza maisha mapya na wewe katika wokovu wa fahamu zangu na mwili. Naitenga damu yangu na kila nguvu ya maamuzi ambayo niliyafanya kwa makosa kwa jina la Yesu.

¤ Bwana, kama kuna namna napitia matatizo ambayo yaliletwa na maamuzi niliyowahi kuyafanya katika maisha yangu naomba leo unitenge na haya maamuzi na athari zake kwa jina la Yesu.

¤ Kila madhabahu inayosema kinyume na mimi leo naifunga kinywa kwa jina la Yesu. Nakataa kuumizwa tena, nakataa majuto.

¤ Hata imekuwa, mtu akiwa ndani ya Kristo amekuwa kiumbe kipya; ya kale yamepita tazama! Yamekuwa mapya. [2 Wakorintho 5:17]
Mimi niko ndani ya Kristo. Kila mambo ya kale yasiyokuwa ya Mungu nayafisha kwa jina la Yesu. Nafisha magonjwa ya kurithi, nafisha umasikini. Nafisha asili ya dhambi na tabia mbaya. Nafisha kila ambacho kinajiinua kinyume na mimi kutokea katika maisha yangu ya zamani kwa jina la Yesu.

■ ENDELEA KUOMBA UKIJUA KWAMBA MUNGU ANASHUGHULIKA NA WEWE.VUNJA KILA NGOME INAYOKUZUIA KUSONGA MBELE AMBAYO MSINGI WAKE NI MAKOSA YAKO YA ZAMANI KWA JINA LA YESU.

MUNGU AKUBARIKI SANA.

Tafadhali watumie maombi haya na ujumbe huu watu wengine na wakaribishe tuombe na kujifunza pamoja. Ikiwa utataka kujiunga na kundi letu la maombi na Neno la Mungu karibu sana.


Discover more from cantonadigital

Subscribe to get the latest posts sent to your email.

Leave a comment