Pasipo maono, watu huacha kujizuia;
Bali ana heri mtu yule aishikaye sheria. (Mithali 29:18)
Kila mtu anahitaji maono, maono ni kama ramani ya ujenzi wa hatma. Kuna mawazo Mungu anamuwazia mtu kabla hajamfanya katika tumbo la mamaye, na kadri mtu huyu anapoongezeka katika hekima na kimo Mungu humtazamisha picha halisi ya maisha yake halisi na hatma yake katika maisha hapa ulimwenguni. Lakini sio rahisi mtu kuishi katika kusudi la Mungu na kutembea katika maono na mawazo ya Mungu mpaka kufikia ile hatma yake humu duniani. Kuna vikwazo na dhiki za kila namna. Roho Mtakatifu yuko kutupa maarifa, ufahamu na hekima ili tuweze kutembea katika mtembeo sahihi kuelekea hatma zetu katika ulimwengu na hatimaye kule mbinguni katika ule ukamilifu wa imani yetu. Wengi wamekata tamaa, wengi adui amezima ndoto zao, wengi wameshindwa nguvu na matatizo, magonjwa na masumbufu ya ulimwengu huu. Wanayo maono na wanajua wanatakiwa kwenda au kushia mahali fulani lakini adui amewaibia nguvu zao, amewasonga na matatizo. Amewafanya wapoteze ujasiri katika kufanya mambo yatakayowasaidia kusogelea kesho zao njema.

Kila shughuli yenye maana hapa ulimwenguni Mungu anayo maono mahsusi kwa ajili yake. Anayo maono kuhusu ndoa, ni kuujaza ulimwengu, ni kuliongeza kanisa la Mungu, ni kujipatia watu wa kufanya nao kazi, ni kuunda mataifa yenye kumhofu yeye na mambo mengine mengi. Anayo maono kwa habari ya huduma za watu , kazi zao, afya zao , uchumi wao na kila eneo la maisha yao. Wengine wanajua maono au mawazo ya Mungu juu yao ila hawajui njia ya kifika, wengine wamefia njiani, wengine wameumizwa na kukata tamaa. Ndugu, unahitaji kutiwa nguvu, unahitaji kuonyeshwa njia, unahitaji kusonga mbele, unahitaji kuonyeshwa silaha na kuelekezwa namna ya kuzitumia.

Discover more from cantonadigital
Subscribe to get the latest posts sent to your email.