Mungu wetu ni Mkuu anajua matukio yote.

MUNGU wetu ni MUNGU anayetangaza mambo ya mwisho tangu mwanzo (Isaya 46:10). Yaani siku zote yeye anatazama unapoelekea na siyo hapo ulipo.

Siku moja katika hali ya ufunuo mtumishi wa Mungu wa kweli, alifundisha kwamba, “Wakati Mungu anawaambia wana wa Israel juu ya nchi yao ya ahadi, aliwaambia kuhusu mema ya nchi hiyo ambayo ni maziwa na asali, lakini hakuwaambia kama njiani kutakuwa na bahari ya shamu na jangwa”.

Hii ndiyo asili ya tabia ya Mungu ambaye jicho lake siku zote hatazami magumu au mabaya inayopitia bali anautazama mwisho mwema na kuutangaza.

Wakati Rebeka anasumbuliwa na uja uzito wake, alipomuomba Mungu kwa ajili ya uponyaji, Mungu alimjibu kuwa, ndani ya tumbo lake kuna mataifa mawili yanashindana (Mwanzo 25:22-23).

Katika macho ya kibinadamu, ama angetumia vipimo vya kitabu vya ultrasound, huyu mama angeonekana tatizo lake linatokana na mimba ambayo ni watoto mapacha, lakini jicho la Mungu, hawakuonekana kama watoto wawili mapacha bali Mungu aliwatazama kama mataifa mawili.

Kwa mujibu wa data za umoja wa mataifa za mwaka 2020 kuhusu hesabu ya waisraeli walioko nchi kwao, ambao hawa ni chimbuko linalotokana na Yakobo (Doto) inaonyesha wako zaidi ya milioni nane na laki sita.

Na idadi ya waedomu ambao ni wa Jordan wa sasa ambao chimbuko lao ni Esau (Kulwa) hawa jamaa wako zaidi ya milioni tisa na laki tano. Hivyo Mungu alipokuwa analitazama tumbo la Rebeka hakuona mapacha bali aliona makundi ya watu zaidi ya milioni kumi na saba wakisumbuana. Huu ndiyo mtazamo wa Mungu katika maisha yetu siku zote.

Katika kitabu cha ufunuo 2:9, tunaona Mungu akimtuma malaika wake kuliambia kanisa la Smirna kwamba, “NAIJUA DHIKI YAKO NA UMASKINI WAKO LAKINI U TAJIRI”.

Hii ina maana kwamba, kila unachokipitia anakijua lakini hatamki jinsi kilivyo kwa sababu hatazami sana yaliyopo, yanayokatisha tamaa ila anatazama mwisho wako wa ushindi juu ya kila changamoto inayokuzunguka.

Inawezekana kabisa hauna, kazi, hauna kodi ya nyumba, hauna pa kuishi, hauna chakula, ama unapita katika mambo magumu kimahusiano, kibiashara, umetengwa, unachukiwa bila sababu. Hayo yote Mungu anayajua na ameyaruhusu yatokee ili mwisho wako uwe mwisho wa ushindi na wenye ushuhuda mkubwa.

Amka popote ulipo usikubali kukatishwa tamaa kwa kuwa mwisho wako ni mzuri mbele za Bwana…….


Discover more from cantonadigital

Subscribe to get the latest posts sent to your email.

Leave a comment