Ni silaha kubwa sana ambayo adui anatumia kuangusha hata majitu ya Imani. Mbaya zaidi dhambi ya kiburi au anguko la kiburi linapokunyemelea, kila Mtu ataona isipokuwa wewe mwenyewe. Hivyo ukiambiwa utaanza kuona watu wanakuonea wivu au wanachuki binafsi na wewe.
Kiburi huwa kinapenya kwa mlango wa kuona umejitambua na sasa unasimamia haki zako za msingi.
“I know who I am, I know my place in God, I am not what people say, I am what God says” (Najijua mimi ni nani, najua nafasi yangu katika Mungu, sipo vile watu wanasema, nipo vile Mungu anasema)
Ni ukiri mzuri sana lakini pia ni hatari sana. Sisemi uishi kwa kufuatisha mawazo ya watu (People’s opinions), la hasha! Ila mara nyingi watu husema kilichopo au kinachokuja.
Kiburi ni ile hali ya kuridhika moyoni kupitiliza, kujiamini kupita unavyopaswa. Mtu mwenye kiburi anaona hata Mungu akimuacha kwa hapo alipofika anaweza kujiendesha mwenyewe. Anaona hamtegemei mtu yeyote wala hamuhitaji mtu yeyote kwenye maisha yake. Ndio mara nyingi husema “hata bila ninyi naweza kufanya peke yangu”. Ukweli ni kwamba hata Mungu aliwahitaji watu kutimiza kusudi lake. Hata Mungu anahitaji mtu wa kusimama mahali palipobomoka, kama Mungu anahitaji watu, vipi wewe mwenzangu na mimi?
DALILI ZA KIBURI.
- UJUAJI.
Mtu mwenye kiburi hakuna unachoweza kumwambia. Hata Ndege anaweza kurusha ukimpa manual book (ndivyo anavyojiona). Huwezi kumwambia kitu yaani ni kama Mungu, ukiwa katika kuwaza ameshajua, kabla hujanena amejibu. Hawezi kukusikiliza mpaka mwisho.
- HAFUNDISHIKI.
Kwa sababu anajua kila kitu moyo wake umeshainuka hawezi kujifunza wala haoni kama anahaja ya kujifunza kitu. Kiukweli huwa anataka kuwa mwalimu wa kila Mtu. Hata akikaa na Baba yake wa kiroho huwa anatamani asikilizwe badala ya kusikiliza akajifunza.
- HAONYEKI
Kwanza ukileta story za kumuonya mnakorofishana kwasababu yupo kwenye njia ya upotovu. Utamwambia nini akusikilize.
- YUKO SAHIHI MARA ZOTE.
Hata akikosea yuko tayari sheria ivunjwe ili yeye Ndio awe sahihi. Hakubali kosa, hata ukimbana atakugeuzia kosa mwenyewe.
Anataka utendaji wake ndio uwe sahihi na mfano wa kuigwa na wengine. Hakubali kama kuna mtu anaweza kuwa bora kama yeye au kumzidi yeye.
- ANAONA MAKOSA KWA KILA MTU.
Mtu mwenye kiburi anaweza kuikosoa hata Biblia. Anaweza kuangalia anga akakwambia Mungu alikosea kuweka anga liwe blue, lilifaa kuwa rangi ya dhahabu.
Hakuna kizuri kwa mtu mwingine yeyote isipokuwa yeye. Hata ungefanya nini huwezi kufikia standards zake.
6.HUJIONA MNYENYEKEVU KULIKO WENGINE.
- HUWA ANAONA AMEKUFANYIA FAVOR KUKUSIKILIZA.
Yaani kuongea na mtu mwingine ni kama amempa mtu Neema kubwa sana.
- ANAONA HAKUNA WA KUFANANA NAYE.
Ukikutana na Mtumishi aliyevamiwa na kiburi anaweza kukwambia dunia nzima hii Mungu alimpa assignment yeye peke yake. Kama Eliya alivyojidanganya kuwa amebaki peke yake asiyepiga goti kwa Baal na Mungu akamuumbua kuwa amejisazia watu 7000, maana yake hata yeye akiasi bado Mungu hakosi mabaki.
- HUTAFUTA FAIDA ZAKE TU.
Kiburi ni kinyume cha unyenyekevu na kiburi ni uhalisia wa roho ya ubinafsi. Mtu mwenye kiburi hata mkienda naye kwenye huduma huwa anataka apewe special treatment kuliko wengine. Atataka Hotel ya peke yake, Mic yake iwe tofauti na wenzake. Kama ni muimbaji kwenye kundi anataka setting yake iwe special. Kila wimbo anataka aongoze yeye. Na hii roho huwa inamfunga mtu hata hajielewi.
Akafungua mdomo kutoa comment lazima atakwaza mtu kwa kumshusha na kujipandisha yeye. Haoni jema kwa wenzake.
- HATAKI USHIRIKIANO.
Ukimuuliza atakwambia kuna kitu special Mungu amempa na akikaa na wenzake watakichafua.
Kiburi kinakufanya kusahau kwa nini meza ya BWANA walishea kikombe. Ile ni kuonesha wote ni kitu kimoja mbele za Mungu. Hakuna aliyebora kuliko mwingine. Hapa simaanishi ujifananishe na Seniors wako kuhuduma lakini mtu asijione yeye ndio badili ya Yesu kwenye maisha ya wengine. Yaani unaweza kuongea naye badala ya Yesu. That is very wrong.
Kristo anabaki kuwa MFALME WA WAFALME kwetu. Hata tukifanya makubwa namna gani tusisahau kuwa ni yeye anayetuwezesha.
Vunja kiburi kwa kunyenyekea. Muombe Mungu macho usijekujikuta umeiendea njia ya Lucifer yule asi na joka la zamani. Shetani hujigeuza malaika wa Nuru, hatakuonesha kosa lako. Ukiona unaumia watu wanapokusema juu ya kitu fulani kichunguze mara mbili. Maana ukijua unasingiziwa ishu ambayo haipo inauma ndio lakini unapuuza ila ukiona kinauma na hakiishi basi kuna namna ukweli upo, shughulika nacho Mtumishi.
Watu wote kweli wanakusingizia wewe tu kuwa unapenda wanawake au unapenda wanaume, unajisikia, unadharau na kila sehemu wakushutumu kwa kitu kimoja tu hicho hicho? Rudi magotini mwombe Mungu msaada kama kipo au kinakunyemelea mwambie akiondoe.
MADHARA YA KIBURI.
- UNAPINGWA NA MUNGU MWENYEWE. (Yakobo 4:6, 1Petro 5:5)
Badala ya kupingwa au kuwekewa vikwazo na mapepo unaanza kupingwa na Mungu mwenyewe. Kila hatua yako inakuwa na upinzani kutoka juu sijui utaponea wapi. Hata uende Nigeria urudi na mafuta ya Upako bado vitu havitaenda kwa sababu Mafuta ya upako hayawezi kumzidi Mungu.
- UNAKUWA CHUKIZO KWA MUNGU.
(Mithali 6:16-17)
Unaingia kwenye orodha ya vitu ambavyo Mungu anavichukia hivyo utumishi wako hauwezi kuwa na thawabu.
- MUNGU ANAKUDHARAU. (Mithali 3:34)
Hii nadhani ndio mbaya zaidi. Yaani unaweza kuwa madhabahuni unaneng’eneka na Mungu anakuona unamkera tu. Kiburi ni kitu kibaya sana.
Unatoa hela kusaidia watu kumbe moyo wako umejaa hila na kutafuta sifa. Mungu aturehemu.
- KIBURI HUKUKOSANISHA NA WATU.
Watu wote wa maana kwenye maisha yako utajikuta unawapoteza kila siku, kila siku unaanza upya, na kila anayeshindwa tabia zako na kuandoka unatengeneza naye bifu. Kwa hivyo kila siku wewe utakuta una vita mpya kila upande. Sasa huku unapingwa na Mungu, huku unagombana na watu, huku unashambuliwa na mapepo ni maisha ya tabu sana.
Nisikuchoshe na maandishi mengi. Jihoji mwenyewe kama upo kwenye njia ya kiburi, unahisi moyo wako imeinuka.
Kama unapenda kusifiwa na kuongelewa vizuri. Kama unatamani kuchukuliwa kipekee. Unataka watu wakupigie magoti ukipita, yaani moyo wako unaburudika. Mtu akikuita kwa jina lako bila kuanza na title, Mtume, Nabii, Baba Askofu, Unahisi, Mheshimiwa, Mchungaji, Baba, yaani unaweza usiitike au unahisi amekudharau. Hapo tayari huo ugonjwa umeanza kutafuna moyo wako.
Ukiombea mtu akapona na wakati wa ushuhuda akamshukuru Mungu bila kukutaja na wewe yaani unaona hana shukurani hiyo pia ni dalili umeshavamiwa na huyu mdudu. Ukitembelea huduma ya mtu mwingine na wasikupe nafasi ya kusalimia unaweza usirudi tena hapo. Ukienda kuhubiri sehemu wasikupokee Biblia yako unaweza ukarudi kwenye gari ukaondoka. Haya yote na mengine mengi ni dalili za kiburi. Yaani ukihubiri na usipate feedback ya ujumbe wako watu wakistaajabia mafunuo, moyo wako unasinyaa.
Kila credit unataka uchukue wewe, lugha yako imetawaliwa na haya maneno, Mimi, yangu, Nikafanya, nikamuombea, unajiweka wewe nafasi ya Mungu.
Unajua nini? WEWE UMESHAACHA KUMTUMIKIA MUNGU ILA UNAJITUMIKIA MWENYEWE NA UKO MBALI KABISA NA NEEMA. NA MWENYE KAZI YAKE ANAKUSHANGAA. NA UNAWEZA KUDHANI MUNGU BADO ANAKUSEMESHA KUMBE NI NAFSI YAKO INAONGEA PAMOJA NA ROHO ZIDANGANYAZO. USIFUMBWE MACHO NA MIUJIZA, HATA WACHAWI WA FARAO WALIGEUZA FIMBO KUWA NYOKA. RUDI MAGOTINI OMBA TOBA NA REHEMA UANZE UPYA NA MUNGU. KIJAPO KIBURI NDIPO UJAPO UHARIBIFU.
Discover more from cantonadigital
Subscribe to get the latest posts sent to your email.