Katika Mapito ufanyeje?

Bwana YESU KRISTO Mwokozi atukuzwe ndugu zangu wote.
Karibuni Sana tujifunze Neno la MUNGU.

Wakati mwingine katika Safari yako ya maisha unaweza kupitia mapito mbalimbali.

Mapito ni nini?
Mapito ni njia ya muda iliyo na magumu ambayo mtu anaipitia.

Mapito ni mambo mabaya magumu ambayo mtu anayapitia.

Mapito ni mambo ambayo huyapendi, usiyoyahitaji ila unayapitia.
Sio kila mtu lazima apitie mapito lakini kama unapitia mapito au kama ulipitia mapito au hata kama utapitia mapito basi jifunze kitu cha msaada kutoka katika somo hili muhimu sana.

Zaburi 142:1-3 ” Kwa sauti yangu nitamlilia BWANA, Kwa sauti yangu nitamwomba BWANA dua. Nitafunua mbele zake malalamiko yangu, Shida yangu nitaitangaza mbele zake. Nilipozimia roho uliyajua MAPITO YANGU; Katika njia niendayo wamenifichia mtego.”

Nimesema sio lazima kila mtu apite katika mapito kama unayopita wewe na sio lazima watu wote wapite katika mapito ya namna moja.
Ni muhimu kujua Cha kufanya ukipitia mapito mbalimbali.

Pito lako linaweza kuwa ni utumwa mzito Kama hawa katika andiko hili.
Kumbu 26:6 Wamisri wakatuonea, wakatutesa, wakatutumikisha utumwa mzito.

Yapo mapito ya aina nyingi.
Kuna watu wanapitia mapito magumu ya kiuchumi, kazi, kibali, mshahara n.k
Kuna watu wanapitia mapito magumu ya kiafya, ajali, magonjwa n.k

Unatakiwa ukae vizuri na MUNGU katika KRISTO YESU ili kwa njia hiyo umfanye MUNGU kuwa adui wa wanaokutesa.
Kutoka 23:22 “Lakini ukiisikiza sauti yake kweli, na kuyatenda yote ninenayo mimi; ndipo mimi nitakuwa ni adui wa adui zako, na mtesi wa hao wakutesao.”

Kuna watu wanapitia mapito ya ndoa, uzao, misiba n.k

Kuna watu wanapitia mapito ya kuonewa, vifungo, kusingiziwa, kudhulumiwa, kuibiwa n.k

Kuna watu wanapitia mapito magumu ya kifamilia,kiukoo,kieneo n.k
Kwa ujumla kuna mapito ya namna nyingi sana.

Kuna aina ya mapito mbalimbali ambayo mtu anaweza akapitia.
Baadhi ya mapito hayo Ni hayo kwa makundi tunaweza kusema hivi;

  1. Mapito kutokana na hila za watu dhidi yako.

Zaburi 10:2 “Kwa kiburi chake asiye haki mnyonge anafuatiwa kwa ukali; Na wanaswe kwa hila zizo hizo walizoziwaza.”

  1. Mapito kutokana na uzembe wako wa kiroho. Hasa uzembe wa kufanya maombi.

Marko 14:38 “Kesheni mwombe, msije mkaingia majaribuni, roho i radhi ila mwili ni dhaifu.”

Inawezekana umejikuta katika matatizo/mapito kwa sababu hukufuata ushauri mzuri, hukumsikiliza ROHO MTAKATIFU, hukufanyia kazi Neno la MUNGU n.k
Umejikuta kwenye njia ya wapumbavu hivyo mapito yako chanzo chake ni wewe kupita katika njia ya wapumbavu kimaamuzi.
Mithali 12:15 “Njia ya mpumbavu imenyoka machoni pake mwenyewe; Bali yeye aliye na hekima husikiliza shauri.”

  1. Mapito kutokana na nguvu za giza/vifungo vya giza/mawakala wa shetani.

Isaya 42:22 “Lakini watu hawa ni watu walioibiwa na kutekwa; wote wamenaswa katika mashimo, wamefichwa katika magereza; wamekuwa mawindo, wala hapana aokoaye; wamekuwa mateka, wala hapana asemaye, Rudisha.”

  1. Mapito kutokana na dhambi zako.

Mithali 1:15-16 ” Mwanangu, usiende njiani pamoja nao; Uzuie mguu wako usiende katika mapito yao. Maana miguu yao huenda mbio maovuni, Nao hufanya haraka ili kumwaga damu.”

Wako watu wako kwenye mapito ya kiafya baada ya kupigwa wakiiba.

Kuna watu walifanya uasherati wakabebeshwa mimba na kutelekezwa.

Kuna watu wengi wako katika mapito magumu sana na vyanzo vya mapito ni dhambi zao.
Dhambi inaweza kuleta mapito yanayoelekea kwenye uharibifu mkubwa.
Mithali 2:18 “Maana nyumba yake inaelekea mauti, Na mapito yake yanakwenda kwenye wafu.”

  1. Mapito kutokana na jaribu la ki MUNGU.

Zaburi 25:4-5 ” Ee BWANA, unijulishe njia zako, Unifundishe mapito yako, Uniongoze katika kweli yako, Na kunifundisha. Maana Wewe ndiwe MUNGU wa wokovu wangu, Nakungoja Wewe mchana kutwa.”

Kukupima kama uko tayari kwa hatua nzuri zaidi na kiroho.
Kukuimalisha n.k

Mfano ni huu.
Ayubu 19:5-9 ” Kwamba mtajitukuza juu yangu, Na kunena juu yangu shutumu langu; Jueni basi kuwa MUNGU amenipotosha, Na kunizingira kwa wavu wake. Tazama, nalia, Udhalimu, lakini sisikiwi; Naulilia msaada, wala hapana hukumu. Yeye ameiziba njia yangu nisipate kupita, Na kutia giza katika mapito yangu. Amenivua utukufu wangu, Na kuiondoa taji kichwani mwangu.”

Je wewe unapitia mapito gani?

=Mapito ya Hannah ilikuwa kukosekana kwa mtoto, lakini alipong’ang’ania kwa MUNGU alipata watoto 6.
1 Samweli 2:21 “Naye BWANA akamwangalia Hana, naye akachukua mimba, akazaa watoto, wa kiume watatu na wa kike wawili. Naye huyo mtoto Samweli akakua mbele za BWANA.”

=Mapito ya Bartimayo ilikuwa upofu, aliloitambua siri ya kupona kwamba ni kumfuata Bwana YESU KRISTO alimfuata na akaponywa.
Marko 10:51-52 ” YESU akamjibu, akamwambia, Wataka nikufanyie nini? Yule kipofu akamwambia, Mwalimu wangu, nataka nipate kuona. YESU akamwambia, Enenda zako, imani yako imekuponya. Mara akapata kuona; akamfuata njiani.”

=Mapito ya Wayahudi kule Babeli ilikuwa kutaka kuuawa kwa hila za Hamani, walipofunga siku 3 Hamani alikufa yeye na sio wao.
Esta 7:10 “Basi wakamtundika Hamani juu ya mti aliomwekea tayari Mordekai. Ghadhabu ya mfalme ikatulia.”

Hata wewe wakati mwingine unaweza ukajikuta katika mapito magumu.
Nakumbuka mimi Cantona wakati nikiwa shule ya upili, kuna Kijana namkumbuka Alikua anaumwa Sana,akapewa mapumziko akalala Bwenini, siku hiyo Bweni yao walishinda watu wawili huku wengine wakiwa darasani. Baadae mchana wanafunzi waliporudi Bwenini,mmoja alikuta ameibiwa pesa yake ya matumizi elfu 13. Kwa sababu kitanda chake hakikuwa mbali Sana na kitanda cha aliyekua akiugua watu wengi wakadhani ni yeye pesa aliyeiba hela hiyo. Aliyeibiwa akaenda kumjulisha Mwalimu wa zamu ambaye ni Mwalimu kijana tu. Yule Mwalimu alilofika tu bila kuuliza chochote alimchapa mbele ya wanafunzi wote yule Kijana uchi uchi maana alisema avae tu kibukta kidogo na awe kifua wazi, alimchapa sana, huku akiwa anaumwa, mwili ukavimba mno kisha akamwambia alale katika kokoto huku mvua kubwa ikimnyeeshea na eneo hilo lilikuwa karibu na Bweni na hapo alipolala ni sehemu ambayo wanafunzi kujisaidia haja ndogo usiku na hupigia miswaki asubuhi. Mvua ilinyesha hadi ikakatika huku wanafunzi wote wa kiume na wa kike wakimtazama, wengine wakmhurumia na wengine wakimcheka na kumwita mwizi. Baada ya adhabu hiyo mbaya sana ya uchi uchi watu wengi walijitenga mbali na yeye ilipofika usiku aliwaza kupanga nguo zake ili niache shule maana rohoni nakiyokua nayo Mwilini kwa sababu ya kusingiziwa, hayo maumivu yalikuwa makubwa Sana. Rafiki yake mmoja aliyekuwa ameokoka aliponiona katika hali hiyo alinikaribia na kuanza kuniambia ” najua hujaiba ila ukitoroka shule ndipo watu wote watadhani wewe ni mwizi, hivyo endelea na shule na MUNGU ataufunua ukweli.”
Ni kweli aliendelea na masomo ila akiwa katika mapito magumu sana kutokana na uongo aliosingiziwa.
Ashukuriwe MUNGU wa mbinguni maana baada ya kama mwezi mmoja aliyeiba aligundulika na pesa ikarudishwa, aliyeiba alikuwa rafiki wa karibu Sana na aliyeibiwa kiasi kwamba hakuna mtu angehisi kama ndiye kaiba.
Wakati huu ndani yake,maumivu ndipo yalizidi Sana japokuwa aliliombwa msamaha na watu wengi akiwemo Mwalimu, aliwasamehe wote.
Aliwasamehe lakini japokuwa hakusahau.

Nimekujulisha jambo hilo ili ujue kwamba wakati mwingine katika hali usiyoidhani unaweza ukapita katika mapito, tambua nini Cha kufanya katika mapito.

Kuna familia walikuwa matajiri wanaoishi maisha Safi lakini siku moja ghafla tu baba wa familia hiyo alifariki, ndugu waligawana Mali na watoto wakagawanwa na kwenda kuteseka kwa ndugu.

Mama mmoja alipofiwa na mumewe ndugu walimsingizia ndiye kamuua mume wake hivyo akafukuzwa na hakupewa Mali hata kidogo.
Mama Yule kilio chake kilikuwa kikubwa kwa muda mrefu Sana. Wakati mwingine alijikuta anaenda kwenye kaburi la mumewe mara kwa mara akiomba MUNGU amfufue ili aje aseme ukweli.
Ndugu kwa hila walizitamani Mali za kaka yao hivyo wakaona njia nyepesi ya kumfukuza shemeji yao ni kumsingizia uchawi, ni ushetani wa hali ya juu Sana.

Ndugu, hata wewe unaweza ukapitia mapito mbalimbali.
Unaweza ukapitia mapito katika ndoa, uchumi, afya, uzao, kazi , kibali n.k

Ndugu, sehemu muhimu zaidi ya somo hili ni hii.
Ufanye nini ukiwa katika mapito?

  1. Ishi maisha matakatifu ili msaada wa KRISTO ufanye kazi kwako.

Mithali 12:28 “Katika njia ya haki kuna uhai; Wala hakuna mauti katika mapito yake.”

  1. Endelea Kumtegemea MUNGU na kumtumainia yeye.

Yeremia 17:7 “Amebarikiwa mtu yule anayemtegemea Bwana, Ambaye Bwana ni tumaini lake.”

  1. Endelea na maombi katika jina la YESU KRISTO kwa Imani.

Zaburi 142:1-3 ” Kwa sauti yangu nitamlilia BWANA, Kwa sauti yangu nitamwomba BWANA dua. Nitafunua mbele zake malalamiko yangu, Shida yangu nitaitangaza mbele zake. Nilipozimia roho uliyajua mapito yangu; Katika njia niendayo wamenifichia mtego.”

  1. Usijilinganishe na watu wasio katika mapito kama wewe wakati huo, Bali mtegemee MUNGU katika KRISTO YESU wakati huo.

Ayubu 19:25 “Lakini mimi najua ya kuwa Mteteaji wangu yu hai, Na ya kuwa hatimaye atasimama juu ya nchi.”

  1. Kama ni mapito ya kujitakia mwenyewe kwa sababu ya dhambi zako au uzembe wako, tubu kwa ajili ya dhambi zako hizo na uziache zote.

Luka 13:3 “Nawaambia, Sivyo; lakini msipotubu, ninyi nyote mtaangamia vivyo hivyo.”

  1. Usilalamike wala kunung’unika wakati ukiwa katika mapito.

Wafilipi 2:14 “Yatendeni mambo yote pasipo manung’uniko wala mashindano,”

  1. Endelea kupambana kiroho hadi ushinde, Kama mapito yako yanasababishwa na nguvu za giza.

Waefeso 6:12 “Kwa maana kushindana kwetu sisi si juu ya damu na nyama; bali ni juu ya falme na mamlaka, juu ya wakuu wa giza hili, juu ya majeshi ya pepo wabaya katika ulimwengu wa roho.”

  1. Usipunguze chochote katika mambo ya ki MUNGU uliyokuwa unayafanya.

1 Wakorintho 15:58 “Basi, ndugu zangu wapendwa, mwimarike, msitikisike, mkazidi sana kutenda kazi ya BWANA sikuzote, kwa kuwa mwajua ya kwamba taabu yenu siyo bure katika Bwana(YESU).”

Kama ulikuwa mtoaji endelea kumtolea MUNGU kwa uaminifu.
Kama ulikuwa unamtumikia Bwana YESU KRISTO endelea kumtumikia kwa uaminifu na juhudi.
Kama ulikuwa unafanya jambo lolote la ki MUNGU usiache bali endelea kufanya hivyo.

Mche MUNGU katika KRISTO YESU Mwokozi na utaitwa heri.
Asante kama umelielewa Neno la MUNGU la siku ya leo ila nina neno moja la mwisho kwako leo.

Bwana YESU Amekaribia Kurudi.

Je, Umejiandaaje?

Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na Bwana YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?

Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee Bwana YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.

Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.

Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.

Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa Bwana YESU Kwako.

Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU.


Discover more from cantonadigital

Subscribe to get the latest posts sent to your email.

Leave a comment