Usikate tamaa maishani.

Mama mmoja alihangaika sana kupata mtoto, katika umri wake wa miaka 45 alikua ameolewa mara tatu na katika kila ndoa aliachika kwakua hakua na uwezo wa kupata mtoto. Baada ya kukata tamaa ya maisha alikuja kukutana na mwanaume mmoja ambaye alimpenda, alimuambia yule mwanaume tatizo lake lakini hakujali, alimuoa katika ndoa ya nne.

Bila kutarajia na wala bila kujaribu kwani alishakata tamaa yule Mama alipata ujauzito na kubahatika kupata mtoto wake wa kwanza akiwa na miaka 45. Hakuamini, alimpenda mwanae na kumlinda kama mboni ya jicho. Lakini wakati mmoja akiwa na miaka50 mume wake wakiwa safarini kwenye gari walipata ajali, ajali ambayo ilipelekea kifo cha mume wake pamoja na mtoto wake wa pekee.

Yalikua ni maumivu makubwa, alikaa ndani mwezi mmoja akilia bila kutoka. Lakini alipotoka yule Mama alienda kutoa sadaka ya kumshukuru Mungu kwa yote yaliyomkuta. Watu walimshangaa ni kwanini katoa sadaka ya kumshukuru Mungu wakati alikua amefiwa na mwanae wa pekee pamoja na mume wake, ndugu wa mume walikasirika na kudhani labda aliamua kuitoa familia yake kama sadaka ya kutafuta mali.

Yule Mama hakujali maneno ya watu ambao walianza kumuangalia kama mchawi hasa baada ya kuanza kufanikiwa katika maisha. Siku moja Mama mkwe wake alikasirika, aliamua kumtolea uvivu kwani mwanzoni walikua wakiongea kimya kimya, alimuuliza ni kwanini alienda kutoa sadaka ya shukurani wakati alifiwa na mtoto na mume wake, alikasirika kwani hata yeye alipoteza mtoto.

Yule Mama alitabasamu na kumuambia “Kuna wanawake wengi ambao wanalia kila siku wakitamani kupata mtoto, mimi nilikua mmoja wao, Mungu akaamua kunipa mtoto kwa miaka mitano. Kuna wanawake wengi ambao wanalia kila siku kwenye ndoa wakiumizwa na waume zao, mimi nilikua mmoja wao katika ndoa tatu, lakini Mungu alinipa mwanao na kunipa ndoa yenye amani kwa miaka mitano.

Sikumshukuru Mungu kwa kuwachukua wapendwa wangu bali nilimshukuru Mungu kwa kunipa miaka mitano ya furaha na amani. Nilimshukuru Mungu kwakua najua wanayopitia wengine, namshukuru Mungu kwani pamoja na kwamba mwanangu leo hayupo lakini bado naitwa Mama wakati kuna wanawake wengi wanatamani kuitwa Mama na hawawezi, kama nisimngeshukuru kwa kidogo basi sikustahili kikubwa!”

NOTE; Unaweza kuwa unapitia katika wakati mgumu na kujikuta unakata tamaa na hata kumlaumu Mungu. Lakini unajua ni watu wangapi wanapitia wakati mgumu kuliko wewe? Kama ungechukua angalau sekunde tano kuangalia maisha ya wengine, ungepiga goti na kumuambia Mungu “Kabla ya kukuomba kuniondolea Kikombe hiki nashukuru kwa Baraka hizi kwani sikukupa chochote kunipa ulichonipa sasa!”


Discover more from cantonadigital

Subscribe to get the latest posts sent to your email.

Leave a comment