Bwana YESU KRISTO atukuzwe ndugu zangu wote.
Karibu tujifunze Neno la MUNGU.
Vipo vitu vingi tu vya kuonekana kwa mtumishi wa MUNGU.
Mtumishi wa MUNGU ndio kiongozi wa kiroho.
Mtumishi wa MUNGU anaweza akaonekana kwa maneno yake, maamuzi yake, msimamo wake au elimu yake ya kiroho.
Mtumishi wa MUNGU anaweza akaonekana kwa mavazi yake, uzoefu katika kazi ya MUNGU au hata anaweza akaonekana kwa mkao wake.
Haijalishi mtumishi anaonekana kwa jambo gani lakini matendo ndio huonekana zaidi.
Watumishi wa MUNGU ni barua inayosomwa na watu wengi Sana.
2 Wakorintho 3:3 “mnadhihirishwa kwamba mmekuwa barua ya KRISTO tuliyoikatibu, iliyoandikwa si kwa wino, bali kwa ROHO wa MUNGU aliye hai; si katika vibao vya mawe, ila katika vibao ambavyo ni mioyo ya nyama.”
Matendo yako Mtumishi ndio barua yenyewe, je barua yako ikije?
Matendo pekee ndio huonekana na kumtambulisha vyema mtumishi wa MUNGU.
Kuna watumishi huwa ni wajuzi sana katika maneno lakini matendo huwaonyesha kwamba sio watumishi wa MUNGU.
Katika jamii ya leo kila mtu anaweza akajiita mtumishi wa MUNGU kwa sababu watu wanamuona anamtumikia MUNGU lakini matendo yake mabaya yanaweza kumuondoa katika kundi la watumishi wa MUNGU.
Hata watumishi walio mapandikizi ya shetani wapo tena wengi tu.
Tito 1:16 “Wanakiri ya kwamba wanamjua MUNGU, bali kwa matendo yao wanamkana; ni wenye machukizo, waasi, wala kwa kila tendo jema hawafai.”
Bwana YESU ametuokoa kwa damu yake ya thamani sana na anataka tulichunge kundi la MUNGU.
Matendo 20:28 “Jitunzeni nafsi zenu, na lile kundi lote nalo, ambalo ROHO MTAKATIFU amewaweka ninyi kuwa waangalizi ndani yake, mpate kulilisha kanisa lake MUNGU, alilolinunua kwa damu yake mwenyewe.”
Sasa kundi la MUNGU wengi kwa sababu ya kutokuzingatia Neno la KRISTO wamejikuta wakichukuliwa na watumishi wasio sahihi.
Usahihi wa mtumishi hauko katika maneno yake tu bali matendo yake yanatakiwa kumthibitisha kwamba kweli yeye ni mtumishi wa MUNGU aliyeokolewa na YESU KRISTO.
Mtumishi wa MUNGU asipojitambua hakika anaweza kulivuruga kundi la MUNGU.
Siku moja nilienda Kanisa fulani kuabudu kwa sababu nilikuwa safarini. Kanisa lile madhabahu yake iko juu kiasi kwamba mtu ukipanda madhabahuni unapanda ngazi, Nikiwa pale Kanisani wakati wa ibada akapanda Mtumishi wa MUNGU mmoja mwanamke ambaye amevaa nguo fupi inayovuka magoti yake, kwa sababu ilikuwa lazima apande madhabahuni basi hata kupanda ilikuwa tatizo maana nguo za ndani zilikuwa zinaonekana wakati anapanda madhabahuni. Akiwa madhabahuni wamama karibia wote kanisani waliangalia chini maana Mwanamke mwenzao aliye mtumishi wa MUNGU alikuwa uchi madhabahuni, kwa muda mfupi niligundua waliokuwa wanamwangalia mtumishi yule ni wanaume zaidi. Yeye hata sijui alikuwa na ufahamu gani maana alishika mic na kusema ‘’Bwana Asifiwe’’ watu waliitikia ‘’Amen’’ kwa sauti huku wakicheka yeye akidhani wanafurahi kumbe wanamcheka na kumshangaa. Niliwaza sana kwa sababu ya mtumishi yule.
Siku moja pia kulikuwa na tamasha la waimbaji wa nyimbo za injili, alipanda mwimbaji mmoja mwenye kipaji wa kike lakini ilikuwa ni aibu ya mwaka. Mwanamke yule ana kipaji cha ajabu cha kuimba lakini siku hiyo alivaa nguo nyekundu fupi sana ambayo ilikuwa fupi inavuka magoti yake, alikuwa na team yake ya waitikiaji ambao wote walivaa vizuri sana kiheshima sana lakini mwimbashaji wao ambaye ndiye huyo staa alikuwa hovyo kabisa. Aliimbisha wimbo wa kuabudu kwa mbwembwe lakini watu hata kuitikia wimbo ule ilikuwa tatizo maana waliona anayeimbisha hafanani na waenda mbinguni.
Watumishi wa MUNGU wengi hawajui kwamba wao ni kielelezo.
Watumishi wengi ni rahisi kuwajua kwamba hawa wanateswa pepo mchafu wa kuipenda dunia na mambo yake hivyo wanahitaji kufunguliwa.
1 Yohana 2:16-17 ” Msiipende dunia, wala mambo yaliyomo katika dunia. Mtu akiipenda dunia, kumpenda Baba(MUNGU) hakumo ndani yake. Maana kila kilichomo duniani, yaani, tamaa ya mwili, na tamaa ya macho, na kiburi cha uzima, havitokani na Baba, bali vyatokana na dunia. Na dunia inapita, pamoja na tamaa zake, bali yeye afanyaye mapenzi ya MUNGU adumu hata milele.”
Kama mchungaji unatukana watu, je unawafundisha nini washirika wako?
Kama Mchungaji ni mwizi unawafundisha nini washirika?
Kama mtumishi wa MUNGU unafumaniwa, je bado utabaki kujiita mpakwa mafuta wa MUNGU?
Biblia inasema ukimwacha MUNGU na yeye atakuacha wewe.
2 Mambo ya Nyakati 15:2 ” ……… BWANA yu pamoja nanyi, mkiwa pamoja naye; nanyi mkimtafuta ataonekana kwenu; lakini mkimwacha atawaacha ninyi.”
Wengi sana MUNGU amewaacha kwa sababu ya matendo yao mabaya.
Mtumishi wa MUNGU inakupasa sana kuliishi Neno la MUNGU.
Mtumishi wa MUNGU inampasa kuwa makini sana katika matendo na usemi.
Kwanini matendo ya mtumishi wa MUNGU au kiongozi wa kiroho yaonekane zaidi kuliko vingine vyote?
Ni kwasababu Matendo huongee zaidi kwa jamii kuliko vitu vingine vyote kwa mtu.
Mathayo 12:33″ Ufanyeni mti kuwa mzuri na matunda yake kuwa mazuri; au ufanyeni mti kuwa mbaya na matunda yake mabaya, KWA MAANA KWA MATUNDA YAKE MTI HUTAMBULIKANA.”
Kazi zako kwa YESU ndizo zinatakiwa kukutambulisha kwamba wewe ni mtumishi wa MUNGU au wewe ni kiongozi mzuri wa kiroho.
Matendo huzungumza zaidi kuliko vitu vingine vyote.
Matendo ndio hubeba kusudi la MUNGU, Wito au kazi uliyoitiwa. 1 Kor 15:58
1 Wakorintho 15:58 “Basi, ndugu zangu wapendwa, mwimarike, msitikisike, mkazidi sana kutenda kazi ya BWANA sikuzote, kwa kuwa mwajua ya kwamba taabu yenu siyo bure katika BWANA.”
Watu wengi hujiita watumishi wa MUNGU, Lakini kazi zao katika injili ya KRISTO ndizo zinatakiwa kuwatambulisha kwamba kweli wao ni watumishi wa MUNGU.
Watu wengi sana kujiita wapakwa mafuta wa MUNGU, Wengine hujiita Manabii, wengine hujiita mitume, wengine hujiita wachungaji au waalimu au wainjilisti lakini kujiita tu haiwezi kukuonyesha kwamba wewe ni mtumishi wa MUNGU.
Watu huangalia kazi zako ndipo watabaini wewe ni Mtumishi wa MUNGU au sio.
Wengine wamevamia huduma za wengine.
Mtu anajua kabisa yeye ameitwa kama mwinjilisti lakini anajiita Nabii na watu hawaoni unabii unaotimia kutoka kwake, huyo watabaini sio mtumishi wa kweli wa MUNGU.
Huwezi ukajiita Mchungaji wakati hujawahi kumuongoza sala ya toba mtu hata mmoja.
Kazi zako katika ufalme wa MUNGU ndio inayoweza kuwajulisha watu kwamba wewe kweli ni mtumishi wa MUNGU.
Kwa matendo yako ndipo watu watamtukuza MUNGU.
Najua uongo wa shetani ni mwingi Sana dhidi ya watumishi wa MUNGU lakini wewe Mtumishi tenda matendo mema siku zote.
1 Petro 2:12 “Mwe na mwenendo mzuri kati ya Mataifa, ili, iwapo huwasingizia kuwa watenda mabaya, wayatazamapo matendo yenu mazuri, wamtukuze MUNGU siku ya kujiliwa.”
Ukiona watu wanamshukuru MUNGU baada ya kujifunza Neno la MUNGU sahihi ujue pia kuna mtumishi wa MUNGU aliyewafundisha Neno hilo.
Sasa kama wewe unajiita nabii au Mtumishi na huku hujawahi kuwafanya watu wamtukuze MUNGU baada ya kufungunguliwa na Neno MUNGU ulilofundisha wewe unahitaji kujiuliza sana.
Injili ya KRISTO ni lazima iambatane na watu kufunguliwa na kupata ufahamu wa kiroho hata wanamtukuza MUNGU kwa ajili yako.
Unatakiwa kufanya juhudi kubwa ili ROHO wa MUNGU akupe ujumbe na ili watu wa MUNGU wafunguliwe na kupata ufahamu sahihi ndipo wamtukuze MUNGU.
Mtumishi wa MUNGU lazima awafanye watu wamtukuze MUNGU katika KRISTO YESU Mwokozi.
Mtumishi wa MUNGU ni lazima awafanye watu wamtukuze Bwana YESU Mwokozi.
Mtumishi wa MUNGU ni lazima awafanye watu wapate ufahamu wa kiroho wa kuwasaidia katika safari ya mbinguni.
Kila mmoja atalipwa kwa matendo yake.
Mathayo 16:27 “Kwa sababu Mwana wa Adamu atakuja katika utukufu wa Baba yake pamoja na malaika zake; ndipo atakapomlipa kila mtu kwa kadiri ya matendo yake.”
Matendo yana nguvu mno na hayo ndio huonekana zaidi na Neno la MUNGU linasema kila mmoja atalipwa sawasawa na matendo yake.
Kama matendo yako ni mema katika KRISTO utalipwa uzima wa milele, kama matendo yako ni mabaya utalipwa jehanamu.
Matendo huongea zaidi ya vyote hivyo katika matendo yako kama mtumishi wa MUNGU inakupasa kuwa makini sana.
Matendo ya dhambi yatakuharibia utumishi wako hivyo inakupasa sana kuwa kielelezo safi katika matendo mema maana wewe u kiongozi wa kiroho.
Matendo ndio kazi yenyewe inayoleta thawabu.
Thawabu ni malipo anayoyapata mtu kutoka kwa MUNGU baada ya kufanya kazi ya MUNGU.
Bwana YESU KRISTO anasema ” Tazama, naja upesi, na ujira wangu u pamoja nami, kumlipa kila mtu kama kazi yake ilivyo.-Ufunuo 22:12″
Kwanini ulipwe sawasawa na matendo yako?
Ni kwa sababu matendo ndio hukuonyesha wewe ni nani.
Matendo huzaa matunda, Bwana YESU KRISTO anasema “Si ninyi mlionichagua mimi, bali ni mimi niliyewachagua ninyi; nami nikawaweka mwende mkazae matunda; na matunda yenu yapate kukaa; ili kwamba lo lote mmwombalo Baba kwa jina langu awapeni.-Yohana 15:16”
Matendo mema katika utumishi wako kutengeneza kibali cha kukubaliwa na watu na kukubaliwa na MUNGU.
Matendo yako kama mtumishi wa MUNGU ni muhimu sana yazae matunda.
Watu kuokoka baada ya wewe kuwahubiri Neno la MUNGU ni sehemu ya matunda mazuri.
Watu kufunguliwa, watu kubadilika tabia kutoka matendo mabaya na sasa Neno lako limewabadilisha na wamekuwa watu wazuri, huko ni kuzaa matunda.
Matendo kwa mtumishi ni muhimu sana maana hayo ndio huzaa matunda.
Mche MUNGU katika KRISTO YESU Mwokozi na utaitwa heri.
Asante kama umelielewa Neno la MUNGU la siku ya leo ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
Bwana YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na Bwana YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee Bwana YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa Bwana YESU Kwako.
CantonaJoseph’s contacts
Facebook https://www.facebook.com/CantonaJoseph/
Instagram https://www.instagram.com/Cantona.Joseph.
Twitter https://twitter.com/@CantonaJoseph
LinkedIn https://www.linkedin.com/in/CantonaJo…
Management Fortune Baraka Entertainments
Website https://CantonaJoseph.Wordpress.Com
Email fortunebaraka.entertainmentsltd@gmail.com
cantona.online254@gmail.com
Contacts +254748836127
Wewe ni wa maana sana!
Copyrights Reserved @2019 FortuneBaraka Entertainments.
Discover more from cantonadigital
Subscribe to get the latest posts sent to your email.